• HABARI MPYA

  Jumanne, Novemba 26, 2019

  AZAM FC YATOA ONYO LIGI KUU, YAWACHAPA ALLIANCE 5-0 CHIRWA APIGA HAT TRICK NYAMAGANA

  Na Mwandishi Wetu, MWANZA
  TIMU ya Azam FC leo imetoa onyo kwa wapinzani kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuwachapa Alliance FC 5-0 Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Meshack Suda wa Singida aliyesaidiwa na Martin Martin Mwalyaje wa Tabora na Leonard Mkumbo wa Manyara mshambuliaji Mzambia, Obrey Choro Chirwa alifunga mabao matatu, huku mengine yakifungwa na Shaaban Iddi Chilunda.
  Chirwa aliye katika msimu wake wa pili Azam FC tangu asajiliwe kutoka Yanga SC, alifunga mabao yake dakika ya nne, 25 na 68, wakati Chilunda alifunga dakika ya 33 na 53.

  Kwa ushindi huo, Azam FC inafikisha pointi 19 katika mchezo wa tisa na kupanda hadi nafasi ya nne, nyuma ya Tanzania Prisons yenye pointi 20 za mechi 12.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Mtibwa Sugar imeibuka na ushindi wa 3-1 ugenini dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Mabao ya Mtibwa Sugar yamefungwa na Juma Nyoso aliyejifunga dakika ya 65, Haruna Chanongo dakika ya 78 na 90 na ushei, wakati bao pekee la Kagera limefungwa na Awesu Awesu dakika ya 39.
  Mwadui FC ikatoka nyuma na kushinda 2-1 dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, mabao yake yakifungwa na Merickiard Mazella dakika ya 65 na Wallace Kiango dakika ya 90 na ushei, baada ya Peter Mapunda kuanza kuwafungia wenyeji kwa penalti dakika ya 44.
  Nayo JKT Tanzania ikautumia vyema Uwanja wa nyumbani, Meja Isamuhyo huko Mbweni, nje kidogo ya Jiji la Darves Salaam kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting. Mabao ya JKT Tanzania yamefungwa na Jabir Aziz dakika ya 15 na Adam Adam dakika ya 17, wakati la Ruvu limefungwa na Rajab Zahir kwa penalti dakika ya 40.
  Na bao pekee la Lenny Kisu dakika ya 57 likaipa Biashara United ushindi wa 1-0 dhidi ya Lipuli FC Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara huku Mbao FC ikiichapa KMC 2-0, mabao ya Waziri Junior dakika ya 81 na Abdulkarim Segeja dakika ya 88 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Kikosi cha Alliance FC kilikuwa; Andrew Ntala, Godlove Mdumile/Zabona Hamisi dk63, Siraj Juma, Erick Mrilo, Wema Sadoki, Juma Nyangi, Sameer Vincent/Shaaban William dk46, Martin Kiggi, Michael Chinedu, Jerson Tegete/Hussein Kasanga dk36 na David Richard.
  Azam FC; Mwadini Ali, NIco Wadada, Bruce Kangwa, Aggrey Morris, Yakubu Mohamed, Mudathir Yahya/Donald Ngoma dk82, Iddi Suleiman ‘Nado’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Abdalah Masoud ‘Cabaye’ dk71, Obrey Chirwa/Abdulkasim Suleman dk73, SHaaban Iddi Chilunda na Joseph Mahundi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YATOA ONYO LIGI KUU, YAWACHAPA ALLIANCE 5-0 CHIRWA APIGA HAT TRICK NYAMAGANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top