• HABARI MPYA

  Friday, November 15, 2019

  MCHEZAJI NA KIONGOZI WA ZAMANI SIMBA SC, OMAR GUMBO AFARIKI DUNIA KUZIKWA LEO KISUTU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIUNGO wa zamani wa klabu ya Simba SC ya Dar es Salaam, Omar Gumbo amefariki dunia jana usiku nyumbani kwake Sinza Mawasiliano mjini Dar es Salaam.
  Taarifa ya familia ya marehemu imesema kwamba Gumbo ambaye kwa wakati tofauti amekuwa kocha na kiongozi wa klabu yake baada ya kustaafu amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi.
  Msiba wa Gumbo aliyewahi pia kuwa Makamu Mwenyekiti wa Simba SC upo nyumbani kwake  Sinza Mawasiliano na mazishi yanatarajiwa  kufanyika Saa 10:00 jioni makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam. 
  Omar Gumbo (wa pili kutoka kulia) alipokuwa Makamu Mwenyekiti wa Simba akipokea zawadi kutoka kwa Waziri wa Michezo wakati huo, Joel Bendera (marehemu pia) 
  Omar Gumbo wa kwanza kulia waliochuchumaa akiwa katika kikosi cha Simba SC mwaka 1977

  Gumbo atakumbukwa zaidi kwa kuwemo kwenye kikosi cha Simba SC kilichotamba miaka ya 1970 na zaidi baada ya kufika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 1974 ikiitoa timu ngumu ya Ghana katika Robo Fainali, Hearts Of Oak kwa jumla ya mabao 2-0.
  Yalikuwa ni mabao ya Sabu na Abdallah 'King' Kibadeni, Wakenya wakimuita Ndululu kutokana na ufupi wake, mjini Accra, yaliyoipa timu hiyo ushindi wa 2-0, kabla ya kuja kulazimisha sare ya bila kufungana mjini Dar es Salaam.
  Hata hivyo, baada ya kushinda 1-0 mjini Dar es Salaam dhidi ya Mehala El Kubra, Simba ilikwenda kufungwa pia 1-0 na Waarabu hao mjini Cairo, hivyo mchezo kuhamia kwenye mikwaju ya penalti, ambako Wekundu wa Msimbazi waling'olewa.
  Gumbo alikuwemo pia kwenye kikosi cha Simba SC kilichowafunga watani wa jadi, Yanga SC 6-0 Julai 19, mwaka 1977 Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) mjini Dar es Salaam, siku ambayo Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ alifunga mabao matatu dakika za 10, 42 na 89, Jumanne Hassan 'Masimenti' mawili dakika za 60 na 73 na lingine, beki Suleiman Sanga akijifunga dakika ya 20.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MCHEZAJI NA KIONGOZI WA ZAMANI SIMBA SC, OMAR GUMBO AFARIKI DUNIA KUZIKWA LEO KISUTU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top