• HABARI MPYA

  Ijumaa, Novemba 22, 2019

  YANGA SC YAENDELEZA WIMBI LA USHINDI LIGI KUU, YAICHAPA JKT TANZANIA MABAO 3-2 LEO UHURU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imeendeleza wimbi la ushindi katika mechi zake za Ligi Kuu ya Tanzania Bara kufuatia jioni ya leo kuichapa JKT Tanzania 3-2 Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 13 katika mchezo wa sita na kujiinua kutoka nafasi ya 15 hadi ya 12 sasa ikilingana kila kitu na Azam FC iliyopo nafasi ya 11 baada ya kucheza mechi saba.
  Yanga SC iliuanza kwa kasi mchezo wa leo na kufanikiwa kupata bao lake la kwanza dakika ya 11, mfungaji Patrick Sibomana akimalizia krosi ya Deus Kaseke kufuatia shambulizi lilioanzishwa na beki Ally Abdulkarim Mtoni ‘Sonso’. 

  Lakini Adam Adam akaisawazishia JKT Tanzania dakika mbili tu baadaye akimtungua kipa Mkenya, Farouk Shikaro kwa shuti la juu baada ya kupokea pasi ya kiungo, Mwinyi Kazimoto.
  Mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uganda misimu miwili mfululizo iliyopita, Juma Balinya akaifungia Yanga SC bao la pili dakika ya 22 akimalizia pasi ya beki wa kulia Juma Abdul.
  Mshambuliaji mpya kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), David Molinga akaifungia Yanga SC bao la tatu dakika ya 35 kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya Damas Makwaya kumchezea rafu Kaseke nje kidogo ya boksi.
  Mshambuliaji Daniel Lyanga akategua mtego wa kuotea wa mabeki wa Yanga kuifungia JKT Tanzania nao la pili dakika ya 45 na ushei akimalizia pasi ya beki Adeyum Saleh Ahmed.
  Kipindi cha pili Yanga SC walicheza kwa kujizuia kuruhusu bao lingine huku wakishambulia kwa tahadhari na wakafanikiwa kuvuna ushindi wa pili mfululizo chini ya kocha mpya na wa muda, Charles Boniface Mkwasa aliyechukua nafasi ya Mkongo, Mwinyi Zahera aliyefukuzwa mwanzoni mwa mwezi.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Farouk Shikaro, Juma Abdul, Jaffar Mohamed, Ally Mtoni ‘Sonso’, Lamine Moro, Papy Kabamba Tshishimbi, David Kaseke, Mapinduzi Balama/Mohamed Issa ‘Banka’ dk50, David Molinga/Abdulaziz Makame dk61, Juma Balinya na Patrick Sibomana/Mrisho Ngassa dk77.
  JKT Tanzania;  Abdulrahman Mohamed, Michael Aidan, Adeyoum Ahmed, Frank Nchimbi, Damas Makwaya, Jabr Aziz, Mwinyi Kazimoto, Rchard Maranya/Hafidh Mussa dk64, Daniel Lyanga, Adam Adam/Anuary Kilemile dk83 na Edward Songo/Mohamed Rashid dk72.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Alliance imeifunga KMC 2-1 Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza,m mabao yake yakifungwa na Geofrey Luseke dakika ya 15 na David Richard dakika ya 30. Luseke tena akajifunga dakika ya 77 kuwapatia bao la kufutia machozi KMC.
  Namungo FC wakapoteza mechi ya kwanza nyumbani msimu huu wakichapwa 3-1 na Coasta Union Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi. Mabao ya Coastal yalifungwa na Mtenje Albano dakika ya 15, Deogratius Anthony dakika ya 76 na Paul Bukaba aliyejifunga dakika ya 90 na ushei huku la Namungo likifungwa na Reliants Lusajo dakika ya 16.
  Kagera Sugar ikaibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Lipuli FC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, mabao yake yakifungwa na Yusuph Mhilu dakika ya 10 na Nassoro Kapama dakika ya 64, huku Paul Nonga akiwafungia wageni kutoka Iringa dakika ya 85.
  Ndanda FC ikapokea kipigo cha 2-0 kutoka kwa Polisi Tanzania ambayo mabao yake yamefungwa na Andrew Chamungu dakika ya 11 na Idd Mobby dakika ya 83.
  Na bao la dakika ya 83 la Samson Mbangula likainusuru Tanzania Prisons kupoteza mechi nyumbani ikilazimishwa sare ya 1-1 na Mwadui FC iliyotangulia kwa bao la Raphael Aroba dakika ya 70 Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC YAENDELEZA WIMBI LA USHINDI LIGI KUU, YAICHAPA JKT TANZANIA MABAO 3-2 LEO UHURU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top