• HABARI MPYA

  Jumamosi, Novemba 23, 2019

  NI KILIMANJARO QUEENS NA KENYA FAINALI CECAFA CHALLENGE WANAWAKE JUMATATU CHAMAZI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TANZANA Bara itakutana na Kenya katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge Wanawake Jumatatu Saa 10:00 jioni Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.
  Hiyo ni baada ya timu hizo kushinda mechi zao za Nusu Fainali ya michuano hiyo leo, Kilimanjaro Queens wakiilaza 1-0 Uganda na Kenya wakiichapa Burundi 5-0 hapo hapo Azam Complex.
  Bao pekee la Kilimanjaro Queens, mabingwa mara mbili mfululizo wa michuano hiyo limefungwa na mshambuliaji wake nyota, Asha Rashid Saada ‘Mwalala’ dakika ya 90 na ushei akimalizia krosi ya Mwanahamisi Omary Shaluwa ‘Gaucho’.
  Kilimanjaro Queens itamenyana na Kenya katika fainali CECAFA Challenge Wanawake Jumatatu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi 
  Asha Rashid ‘Mwalala’ ameifungia bao pekee Kilimanjaro Queens leo ikiilaza Uganda 1-0

  Na mabao ya Kenya dhidi ya Burundi iliyochapwa pia 5-0 na Tanzania Bara katika mechi ya Kundi A yamefungwa na Dorcus Nixon dakika ya 14, Jentrix Shikangwa dakika ya 53 na 71, Mwanalima Jereko dakika ya 67 na Carazone Aquino dakika ya 87.
  Saa 8:00 mchana Jumatatu Burundi itaanza kumenyana na Uganda katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu kabla ya fainali kufuatia Saa 10:00 jioni.
  Kikosi cha Tanzania Bara kilikuwa; Naitaj Idrisa, Happynes Hezron, Amina Ali, Deonisia Minja, Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’, Stumai Abdallah/Opa Sanga dk89, Julitha Aminiel, Diana Lucas/Enekia Kasonga dk62, Asha Rashid ‘Mwalala’, Fatuma Issa na Asha Shaaban.
  Uganda; Ruth Aturo, Viola Namuddu, Asia Nakibuka, Nabisaalu Bridget, Shadia Nankya, Retica Nabbossa, Aisha Namukisa, Hasifah Nasuuna, Fazila Ikwaput, Juliet Nalukenge na Faudhia Najjemba.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NI KILIMANJARO QUEENS NA KENYA FAINALI CECAFA CHALLENGE WANAWAKE JUMATATU CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top