• HABARI MPYA

  Jumapili, Novemba 24, 2019

  SAMATTA ATOLEWA KRC GENK IKILAZIMISHA SARE YA 2-2 UGENINI KATIKA LIGI YA UBELGIJI

  Na Mwandishi Wetu, MOUSCRON
  MSHAMBULAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jana amecheza kwa dakika 72 kabla ya kupumzishwa klabu yake, KRC Genk ikilazimisha sare ya 2-2 ugenini katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji dhidi ya Royal Excel Mouscron Uwanja wa Le Canonnier mjini Mouscron.
  Samatta alitolewa zikiwa zimebaki dakika 18 na nafasi yake ikachukuliwa na mshambuliaji Mnigeria Stephen Odey wakati huo tayari timu hizo zikiwa zimefungana mabao 2-2.
  Mabao ya Genk iliyokuwa inacheza mechi ya kwanza chini ya kocha wa muda, Domenico Olivieri baada ya kumfukuza Felice Mazzu, yalifungwa na Sébastien Dewaest dakika ya 20 na Pau Onuachu dakika ya 55, wakati ya Mouscron yalifungwa na Stipe Perica dakika ya tatu na Nemanja Antonov dakika ya 66.

  Samatta jana amecheza mechi ya ya 175 jumla kwenye mashindano yote tangu ajiunge na KRC Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akiwa amefunga mabao 69.
  Katika ligi ya Ubelgiji pekee hiyo inakuwa mechi ya 137 akiwa amefunga mabao 53, kwenye Kombe la Ubelgiji amecheza mechi tisa na kufunga mabao mawili, katika Super Cup mechi moja, Ligi ya Mabingwa Ulaya mechi nne mabao mawili na Europa League mechi 24 na mabao 14.
  Kikosi cha KRC Genk kilikuwa; Coucke, Maehle, Dewaest, Cuesta, De Norre, Berge, Heynen/Onuachu dk44, Hrosovsky, Ito, Samatta/Odey dk72 na Paintsil/Bongonda dk80.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA ATOLEWA KRC GENK IKILAZIMISHA SARE YA 2-2 UGENINI KATIKA LIGI YA UBELGIJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top