• HABARI MPYA

  Jumamosi, Novemba 30, 2019

  MWAKINYO AMSHINDA MFILIPINO KWA POINTI, KIDUKU ASHINDA TKO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BONDIA Mtanzania, Hassan Mwakinyo amefanikiwa kutetea taji lake la UBO International uzito wa Super Welter baada ya kumshinda Mfilipino, Arnel Tinampay kwa pointi katika pambano la raundi 10 usiku wa jana Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
  Jaji wa kwanza alitoa pointi 97-93, wa pili akatoa 98-92 wote wakimpa mshindi bondia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 24 na wa tatu akatoa 96-96 kwa maana ya sare.
  Hilo linakuwa pambano la 16 kwa Mwakinyo kushinda kati ya 18, mengi mawili akipoteza tangu aanze ngumi za kulipwa miaka minne iliyopita pambano lake la kwanza akimshinda Alibaba Ramadhani kwa pointi ukumbi wa Tangamano, Tanga Novemba 29, mwaka 2015.  Katika mapambano ya utangulizi, Twaha Kassim Rubaha ‘Twaha Kiduku’ alipeperusha vyema bendera ya Tanzania baada ya kufanikiwa kumshinda France Ramabolu wa Afrika Kusini kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya tatu uzito wa Super Welter pia.
  Na katika pambano baina ya wapinzani wa kitongoji kimoja, Mabibo na walioibukia katika gym moja, Mfaume Mfaume aliibuka mbabe wa Keisi Ally kwa ushindi wa pointi za majaji wote pambano la raundi nane uzito wa Welter.
  Wakati huo huo: Watu wawili wamefariki na wanane wamejeruhiwa katika ajali ya gari la timu ya Coastal Union iliyokuwa imebeba mashabiki wa ngumi waliokuwa wakitoka kutazama pambano la bondia Hassan Mwakinyo dhidi ya Arnel Tinampay lililofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam usiku wa jana. 
  Ajali hiyo imetokea eneo la Kerege wilayani Bagamoyo, wakati mashabiki hao walipokuwa safarini kurejea jijini Tanga. .
  Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Coastal Union Hafidh Kido imewataja waliofariki kuwa ni Ibrahim Omar na Hussen Saleh ambapo uongozi wa Coastal kwa kushirikiana na ndugu zao, wanafanya taratibu za kuwasafirisha kwenda Tanga kwaajili ya maziko.
  Hadi sasa miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo na majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.

  "Majeruhi walikuwa wanane, mmoja hali yake ilibadilika amepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, na mwingine tumemkuta hapa anaitwa Aziza, ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kwakaheza mkoani Tanga. Abiria wengine tayari wamerejea Tanga wakiwa pamoja na dereva wa gari letu," imeeleza taarifa ya Kido. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MWAKINYO AMSHINDA MFILIPINO KWA POINTI, KIDUKU ASHINDA TKO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top