• HABARI MPYA

  Friday, January 23, 2009

  Simba SC yasubiri mamilioni ya Henry Joseph, Emeh Izuchukwu

  Kiungo Henry Joseph, Mungu mbariki apate ulaji Norway


  KLABU ya Simba ya Dar es Salaam inaweza kupokea donge nono la fedha kutoka klabu ya
  Molde FK ya Norway, iwapo wachezaji wake kiungo Henry Joseph na mshambuliaji Emeh Izuchukwu, raia wa Nigeria watafuzu majariibo katika klabu hiyo.
  Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela, alisema jana kwamba wachezaji hao wanatarajiwa kuondoka nchini keshokutwa kwenda Norway kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika klabu inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ya Molde FK.
  Henry ambaye pia ni Nahodha wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, amepata nafasi hiyo baada ya kiwango chake cha soka kumvutia wakala mmoja anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
  Klabu hiyo ya Molde FK ambayo inashika nafasi ya tisa katika msimamo wa ligi nchini humo yenye timu 14, mwaka jana iliwahi pia kuwaita kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa wachezaji Uhuru Suleiman na Suleiman Ndikumana wa Burundi baada ya kufanya vizuri katika michuano ya Challenge yaliyofanyika mjini, Dar es Salaam.
  Akizungumzia kuondoka kwa Henry, Kocha Mkuu wa Stars, Mbrazil Marcio Maximo, alisema kwamba kiungo huyo atakosa mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Zimbabwe, ambayo imepangwa kufanyika Februari Mosi mwaka huu hapa nchini.
  Lakini atakuwamo katika kikosi kitakachokwenda Ivory Coast katika fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika, (CHAN), zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani pekee.
  Katika michuano hiyo, Stars iliyofuzu baada ya kuzitoa Kenya, Uganda na Burundi, imepangwa katika kundi A, sambamba na wenyeji, Ivory Coast, Senegal na Zambia.
  Kundi B la michuano hiyo linaundwa na timu za Ghana, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC), Libya na Zimbabwe.
  Tangu Maximo aitwe kuifundisha Stars mwaka 2006, hajawahi kumwacha Henry katika kikosi chake na alimkabidhi mikoba ya Unahodha kutoka kwa Mecky Mexime, aliyestaafu soka ya kimataifa.
  Henry akifanikiwa katika majaribio hayo, atakuwa mchezaji wa tano tangu Maximo aanze kufundisha Stars, kupata timu nje.
  Wengine ni kipa Ivo Mapunda anayechezea St George ya Ethiopia, kiungo mshambuliaji Said Maulid ‘SMG’ anayechezea Onze Bravos de Marquis ya Angola na mshambuliaji Danny Mrwanda wa Al Tadhamon ya Kuwait.
  Mrwanda alichukuliwa kwenye timu hiyo kwa pamoja na kiungo Nizar Khalfan, ambaye hata hivyo baada ya Mkataba wake wa mwaka mmoja kumalizika alitemwa na kurejea Tanzania.
  Wakati Mrwanda akiendelea kung’ara Kuwait, Nizar alijiunga na klabu ya Moro United baada ya kurejaa nchini, ingawa baadaye iliropitiwa alikwenda China kukutana na klabu moja ya Uingereza, kwa ajili ya kufanya majaribio ya kuicheza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: Simba SC yasubiri mamilioni ya Henry Joseph, Emeh Izuchukwu Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top