• HABARI MPYA

  Jumatatu, Februari 20, 2017

  YANGA WAINGIA KAMBINI KIGAMBONI LEO

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MABINGWA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC wameingia kambini Kigamboni, Dar es Salaam leo kwa maandalizi ya mchezo wao dhidi ya mahasimu, Simba Jumamosi wiki hii.
  Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba kikosi kimeingia kambini katika majengo maalum ya kukodisha.
  “Timu imeingia kambini leo jioni Kigamboni katika apartments fulani, kujiandaa na mchezo wa Jumamosi,”alisema.
  Yanga inaingia kambini ikitoka kufuzu Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuitoa Ngaya Club de Mde kwa jumla ya mabao 6-2 

  Alipoulizwa sababu za kutokwenda Pemba kama ilivyopangwa awali, Sanga alisema kwamba wameamua kubadilisha mawindo yao.
  “Hatuwezi kila siku kumuwinda mnyama (Simba) kwa staili ile ile, maana yake atashituka na tutamkosa, safari hii tumebadilisha staili na Jumamosi lazima tumuue tena,”alisema Sanga.
  Wakati Yanga wakiingia kambini Kigamboni leo, mahasimu wao Simba wapo Zanzibar tangu Ijumaa wakijiandaa na mchezo wa Jumamosi.
  Kihistoria Kigamboni ni sehemu nyingine yenye kumbukumbu nzuri kwa Yanga, kwani kila ilipokuwa ikiweka kambi huko ilikuwa ikiwafunga mahasimu.
  Miaka ya 1990 Yanga ilikuwa inaweka kambi Chuo cha Sayansi ya Jamii (sasa Chuo cha Mwalimu Nyerere) na mara zote iliifunga Simba ikitokea huko.
  Yanga inaingia kambini Kigamboni ikitoka kufuzu Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuitoa Ngaya Club de Mde kwa jumla ya mabao 6-2, ikishinda 5-1 mjini Moroni Jumapili ya wiki iliyopita, kabla ya kulazimishwa sare ya 1-1 Jumamosi ya juzi Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA WAINGIA KAMBINI KIGAMBONI LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top