• HABARI MPYA

    Friday, February 24, 2017

    'MESSI' AIPELEKA AZAM ROBO FAINALI KOMBE LA TFF

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    BAO pekee lililofungwa na winga Ramadhan Singano ‘Messi’ limetosha kuwaua Mtibwa Sugar na kuipeleka Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, katika robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au michuano ya Azam Sports Fedaration Cup (ASFC).
    Mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa Azam Complex, ulikuwa ni mkali na wa aina yake kwa timu zote kuonyeshana upinzani, ambapo Azam FC ilionekana kucheza vema kwa kipindi kirefu kabla ya Mtibwa Sugara kuibuka dakika 20 za mwisho.
    Azam FC ilianza mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la mapema dakika ya sita likifungwa na Singano, aliyegongeana vema na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ambaye aliendeleza kuwango kizuri katika mtanange huo.
    Ramadhani Singano 'Messi' akipongezwa na wenzake baada ya kufunga bao pekee leo

    Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi waliendeleza kasi yao ili kusaka mabao zaidi, lakini safu ya ulinzi ya Mtibwa Sugar ilikuwa makini kumdhibiti mshambuliaji pekee aliyekuwa amesimamishwa mbele, Yahaya Mohammed, kila alipogusa mpira.
    Matajiri hao wa Azam Complex, walilazimika kufanya mabadiliko dakika ya 41 kufuatia Yahaya kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo huo, ambapo nafasi yake ilichukuliwa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’, ambaye amerejea uwanjani baada ya kukosa mechi nne zilizopita kufuatia kuwa majeruhi.
    Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Azam FC iliondoka uwanjani na uongozi wa bao hilo, ambapo kipindi cha pili ilianza tena kwa kasi ikitaka kupata bao jingine, lakini ilikutana na upinzani mkali kutoka safu ya ulinzi ya Mtibwa iliyokuwa ikiongozwa na Salim Mbonde, aliyekuwa akishirikiana na Dickson Daudi.
    Beki Bruce Kangwa, anayesherehekea siku yake ya kuzaliwa leo, alikosa bao la wazi dakika ya 48 baada ya kupiga shuti lililombabatiza kipa wa Mtibwa Sugar, Said Mohamed.
    Kuelekea dakika 24 za mwisho Azam FC iliongeza nguvu kwenye kikosi chake kwa kufanya mabadiliko ya wachezaji wawili, wakiingia Erasto Nyoni na Masoud Abdallah na kutoka Kangwa na Frank Domayo,
    Licha ya Mtibwa Sugar kufanya mashambulizi kadhaa kuelekea dakika za mwisho za mchezo huo, ilikutana na upinzani mkali kutoka kwa kipa wa Azam FC, Aishi Manula na mabeki wake, Yakubu Mohammed, Aggrey Morris, Shomari Kapombe na Gadiel Michael.
    Mara baada ya mchezo huo, kikosi hicho kitapumzika siku mbili kesho na Jumapili kabla ya kurejea mazoezini Jumatatu jioni kuanza maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Stand United utakaofanyika Machi 4 mwaka huu.
    Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gadiel Michael, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Himid Mao, Ramadhan Singano, Frank Domayo/Abdallah Masoud dk79, Yahaya Mohammed/John Bocco dk41, Salum Abubakar, Bruce Kangwa/Erasto Nyoni dk66.
    Mtibwa Sugar; Said Mohammed, Rodgers Gabriel, Issa Rashid 'Baba Ubaya', Salum Abdallah, Dickson Daudi, Shaaban Nditi, Ally Makarani, Ibrahim Rajab 'Jeba'/Mohammed Issa dk53, Rashid Mandawa/Stahmili Mbonde dk57, Jaffar Salum na Haroun Chanongo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: 'MESSI' AIPELEKA AZAM ROBO FAINALI KOMBE LA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top