• HABARI MPYA

  Jumapili, Februari 26, 2017

  MAVUGO AWAPA AHADI NZURI SIMBA SC

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa Simba, Mrundi Laudit Mavugo amesema kwamba ataendelea kufunga mabao hadi kutimiza ndoto za kuipa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara timu yake hiyo.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo, siku moja baada ya kuisaidia Simba kushinda 2-1 dhidi ya mahasimu, Yanga, Mavugo alisema kwamba alidhamiria kufunga jana.
  “Nilidhamiria kufunga jana na nilijua mabeki wa Yanga watanikaba sana, lakini nilisema nitapigana hadi nifunge na ninashukuru Mungu nimefunga,”alisema.
  Mavugo jana amefikisha mabao saba akiachwa mbali na Simon Msuva wa Yanga, anayeongoza kwa mabao yake 11, akifuatiwa na Shiza Kichuya wa Simba 10, Mbaraka Yussuf wa Kagera Sugar na Amissi Tambwe wa Yanga wenye mabao tisa, Donald Ngoma, Obrey Chirwa wa Yanga, John Bocco wa Azam, Rashid Mandawa wa Mtibwa Sugar na Abdurahman Mussa wa Ruvu Shooting wenye mabao nane kila mmoja.
  Mavugo aliirudisha mchezoni Simba kwa kuifungia bao la kusawazisha dakika ya 66 akiunganishwa kwa kichwa krosi ya Shizza Kichuya, baada ya Simon Msuva kuanza kuifungia Yanga dakika ya tano kwa penalti. 
  Kichuya akaifungia Simba bao la ushindi dakika ya 81 kwa shuti la umbali wa mita 20 na kuinua shangwe za mashabiki wao, licha ya kucheza pungufu tangu dakika ya 57 baada ya Janvier Besala Bokungu kutolewa kwa kadi nyekundu.
  Ushindi huo unaifanya Simba ifikishe pointi 54 baada ya kucheza 23, ikiendelea kuongoza Ligi mbele ya mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 49 za mechi 22.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MAVUGO AWAPA AHADI NZURI SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top