• HABARI MPYA

  Alhamisi, Februari 23, 2017

  STAND UNITED WAPEWA ONYO LA MWISHO KUPULIZIA DAWA VYUMBA VYA TIMU PINZANI KAMBARAGE

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BODI ya Kusimamia na Kuendesha Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imeionya klabu ya Stand United kwamba desturi ya kupulizia dawa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo vya wapinzani wao ikiendelea itaufungia Uwanja wa Kambarage, Shinganga.
  Katika kikao chake cha mwanzoni mwa wiki hii na kufanya tathmini ya mambo mbalimbali yaliyotokea kwenye michezo mbalimbali ya Ligi Kuu ya Vodacom, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili Bodi imeitaka Stand kuwa makini na hilo.
  "Mechi namba 170 (Stand United FC vs Majimaji). Majimaji iliwasilisha malalamiko kuwa chumba chao kubadilishia nguo (changing room) kilipuliziwa na timu pinzani dawa ambayo ni sumu, hivyo kushindwa kukitumia wakati wa mapumziko,"imesema taarifa ya TFF leo. 
  Bodi pia imeagiza Stand United FC pamoja na Meneja wa Uwanja waandikiwe barua kuwa vitendo hivyo vikiendelea kujitokeza uwanja huo utafungiwa kwa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom. 
  Msimamizi wa Kituo ametakiwa kuandikia taarifa yake kuhusu tukio hilo. Pia Daktari wa Uwanja, Dk. Abel Kimuntu ametakiwa kuwasilisha taarifa yake ya kitaalamu kuhusu suala hilo, vilevile Meneja wa Uwanja huo, Meja mstaafu Mohamed Ndaro naye ametakiwa kuwasilisha taarifa yake kuhusu tuhuma hizo za kumwaga dawa kwenye vyumba. 
  Aidha, Bodi imeagiza baada ya mechi namba 17 baina ya Ruvu Shooting na Azam Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, wenyeji Ruvu Shooting iandikiwe barua kuhusu ubovu wa uwanja wake eneo la kuchezea (pitch) ambapo kuna mashimo, hivyo wafanyie marekebisho.
  Bodi pia imesema Polisi Morogoro imepigwa faini ya Sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika 20 kwenye mechi namba 49 dhidi ya Kinondoni Municipal Council (KMC FC), kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(9) ya Ligi Daraja la Kwanza. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(48) ya Ligi Daraja la Kwanza.
  Mchezaji Boniface S. Nyagawa wa Mbeya Warriors amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa kutoa lugha ya matusi kwa Mwamuzi Msaidizi Namba Moja kwenye mechi namba 52 dhidi ya Njombe Mji, tukio lililosababisha atolewe kwenye benchi kwa kadi nyekundu. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 37(7).
  Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, Enock Mwanyonga, na Mwamuzi Msaidizi Namba Mbili, Abdulaziz Ally wameondolewa kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi Daraja la Kwanza baada ya kushindwa kumudu mechi namba 49 kati ya Polisi Mara na Singida United FC.
  Uamuzi huo umefanywa kwa mujibu wa Kanuni ya 38(1a) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.
  Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, Omari Miyala, na Mwamuzi Msaidizi Namba Mbili, Innocent Mwalutanile wamefungiwa miaka miwili kwa kushindwa kumudu mchezo namba 56 kati ya Singida United na Alliance Schools FC.Uamuzi dhidi yao umezingatia Kanuni ya 38 (1a) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.
  Naye Kamishna Hamisi Kambi ameondolewa kwenye orodha ya Makamishna wa Ligi Daraja la Kwanza kwa kushindwa kutoa taarifa ya mchezo huo kwa usahihi. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 39(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Kamishna/Mtathmini Waamuzi.
  Klabu ya Alliance Schools FC imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kugoma kuingia kwenye chumba vya kubadilishia nguo, hivyo kusababisha timu yao ikaguliwe kwenye gari. Adhabu imezingatia Kanuni ya 14(48) ya Ligi Daraja la Kwanza.
  Mechi namba 27 (Bulyanhulu FC vs Mashujaa). Klabu ya Bulyanhulu FC imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) baada ya timu yake kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili. 
  Waamuzi wa mechi hiyo; Mwamuzi Elikana E. Mhoja (Mwanza), Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, John Mrisho (Mwanza), na Mwamuzi Msaidizi Namba Mbili, Mukhusin I. Abdallah wa Mwanza wameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa kushindwa kumudu mchezo huo. Uamuzi dhidi yao umezingatia Kanuni ya 38(1a) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Udhibiti wa Waamuzi. 
  Pia timu ya Bulyanhulu FC ilichelewa kufika kwenye kikao hicho katika mechi namba 28 dhidi ya Milambo FC iliyofanyika kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora. 
  Mechi namba 30 (Mawenzi Market vs Sabasaba United). Klabu ya Mawenzi Market imepigwa faini ya sh. 100,000 (laki moja) kwa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) ikiwa na maofisa wawili tu badala ya wanne, na pia kutokuwa na vifaa vya mchezo. Adhabu dhidi ya klabu ya Mawenzi Market imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili.
  Mchezaji Awadh Ahmed wa Sabasaba United amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kumsukuma Mwamuzi na kugoma kutoka uwanjani baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 37(7) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.
  Malalamiko ya Alliance Schools FC kupinga matokeo ya mechi yake dhidi ya Singida United kwa madai mabao mawili waliyofungwa si halali, na mchezo huo urudiwe kwenye uwanja huru (neutral) yametupwa. 
  Msingi wa kutupa malalamiko hayo ni kuwa matokeo ya uwanjani hayawezi kubadilishwa kwa sababu ya kupinga mabao yaliyofungwa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: STAND UNITED WAPEWA ONYO LA MWISHO KUPULIZIA DAWA VYUMBA VYA TIMU PINZANI KAMBARAGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top