• HABARI MPYA

  Thursday, February 23, 2017

  TOTO YAIMARISHA BENCHI LA UFUNDI, FULGENCE KOCHA MKUU

  Na Mwandishi Wetu, MWANZA
  KIUNGO wa zamani klabu ya Pamba ya Mwanza, Fulgence Novatus ameteuliwa kuwa kocha Mkuu wa Toto Africans ya mjini humo.
  Novatus ametambulishwa leo kuwa kocha Mkuu wa timu hiyo, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na kocha mkongwe, Rogasian Kaijage Oktoba mwaka jana.
  Akizungumza baada ya kukabidhiwa mikoba ya kufundisha timu hiyo, Novatus anayetokea Polisi Mara alisema kwamba atajitahidi kadiri ya uwezo wake kuiwezesha Toto kubaki Ligi Kuu.
  Navatus, kiungo wa zamani wa Lumumba Rovers, alisema atahakikisha katika mechi saba zilizobaki za Ligi Kuu, anaiwezesha Toto kushinda nne na kwamba hizo nyingine atajitahidi pia kushinda.
  Fulgence Novatus (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari leo wakati wa utambulisho wake na picha ya chini akivaa jezi ya Toto
  Alisema anafahamu changamoto zote zinazoikabili Toto kwa sasa, lakini atashirikiana na uongozi, Maofisa wenzake katika benchi la Ufundi na wachezaji kuhakikisha wanaibakiza Ligi Kuu Toto.
  Kwa upande wake, Nahodha Salum Chukwu alisema kwamba wanampokea kwa mikono miwili kocha Novatus na watampa ushirikiano wa kutosha.
  Pamoja na hayo, Chukwu ambaye ni beki, aliitupia lawama safu ya ushambuliaji ya Toto kwamba  ubutu wake ndiyo umesababisha timu sasa inapambana kuepuka kushuka daraja.
  Waziri Junior, mmoja wa washambuliaji wa Toto kwa sasa, alikubali changamoto hiyo na kusema watajibidiisha kuanzia sasa waanze kufunga kwa wingi.
  Kwa sasa Toto inashikia nafasi ya 14 katika Ligi ya timu 16, ikiwa na pointi 22 baada ya kucheza mechi 23, mbele ya Maji Maji ya Songea yenye pointi 22 za mechi 23 pia na JKT Ruvu pointi 20 za mechi 24.
  Timu tatu zitashuka kuzipisha Njombe Mji, Singida United na Lipuli ambazo zimekwishapanda Ligi Kuu. Na Novatus anaungana na Mkurugenzi wa benchi la Ufundi, Mjerumani, Tim Jost na Meneja, Khalfan ‘Babu’ Ngasa kujaribu kuinusuru Toto.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TOTO YAIMARISHA BENCHI LA UFUNDI, FULGENCE KOCHA MKUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top