• HABARI MPYA

    Friday, February 17, 2017

    MWANJALI: SIMBA NA YANGA BONGE LA MECHI LA MAHASIMU AFRIKA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    BEKI wa kati tegemeo wa Simba, Method Mwanjali amesema kwamba Simba na Yanga ni moja ya mechi kubwa za wapinzani wa jadi barani Afrika.
    Akizungumza katika mahojiano maalum na Bin Zubeiry Sports – Online jana mjini Dar es Salaam, Mwanjali alisema kwamba zinapokutana timu hizo kila kitu husimama Tanzania na anafurahi kuwa sehemu ya changamoto hiyo.
    “Zinapokutana Simba na Yanga, wachezaji kwa wachezaji tunafahamiana, wachezaji wa Simba tunawafahamu wachezaji wa Yanga, na wachezaji wa Yanga wanatufahamu wachezaji wa Simba. Inakuwa mechi kali, lakini mwisho wa siku timu bora inashinda,”alisema.

    Hadi sasa, Mwanjali amecheza mechi mbili za mahasimu wao jadi wa soka ya Tanzania, ya kwanza timu hizo zikitoka sare ya 1-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika Ligi Kuu Oktoba 1, mwaka jana na nyingine Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi Janauri 10, mwaka huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar Simba ikishinda kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90.
    Kuelekea kwenye mechi ya marudiano ya Ligi Kuu dhidi ya Yanga, Februari 25, Mwanjali amesema kwamba anatarajia ushindani mkali, lakini lengo lao ni kushinda.
    Pamoja na kufurahia kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwezi Novemba, lakini Mwanjali amesema kwamba anataka kushinda mataji na klabu.
    “Nataka kushinda mataji na timu, na nadhani hicho ndicho kitaleta furaha kubwa na kumbukumbu nzuri kwangu,”alisema.
    Mwanjali alisema kwamba baada ya kucheza nyumbani kwao, Zimbabwe na Afrika Kusini anafurahi sasa amekuja Tanzania kupata uzoefu mpya wa maisha ya soka.
    Ameisifu Ligi Kuu ya Vodacom ni kubwa, nzuri na ina ushindani mkubwa ikiundwa na timu nzuri zinazofanya kila mechi iwe ngumu iwe unacheza na Yanga, au Mbao.
    Pamoja na hayo, Mwanjali amewashauri wadhamini wa Ligi Kuu, kampuni ya Vodacom Tanzania kuboresha udhamini wao katika ligi hiyo ndani ya miaka mitano ijayo, ili kukuza thamani yake.
    Amewaahidi mashabiki wa Simba kuendelea kujituma ili aendelee kufanya vizuri na kuisaidia zaidi klabu yake, hatimaye itimize ndoto za kutwaa mataji.
    Method Mwanjali aliyezaliwa Aprili 25, mwaka 1983 mjini Hwange, Zimbabwe yupo katika msimu wake wa kwanza Simba SC baada ya kujiunga nayo Julai mwaka jana akitokea CAPS United ya kwao.
    Pia amecheza kwa mafanikio Mamelodi Sundowns, Mpumhalanga Aces za Afrika Kusini, Shabanie Mine na Hwange FC za Zimbabwe.
    Amekuwa beki tegemeo na Nahodha wa timu ya taifa ya Zimbabwe. Alikuwa Nahodha wa The Warriors mwaka 2011 chini ya kocha gwiji wa soka ya Zimbabwe, Norman Mapeza kwenye mechi za kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2012. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWANJALI: SIMBA NA YANGA BONGE LA MECHI LA MAHASIMU AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top