• HABARI MPYA

    Sunday, May 01, 2016

    KAMUSOKO NA NGOMA WANGEKUWA AKINA FULANI, MBONA TUNGEKOMA!

    WACHEZAJI adimu zaidi katika soko la Ulaya ni wa kutoka Afrika Mashariki na Kati na si uadimu wa ghali, bali ni kutokuwa na soko huko.
    Wachache, tena sana wanabatika kucheza na Ulaya na hao ukisoma historia zao ni ambao hawajaathirika na malezi ya kwetu.
    Victor Wanyama, kiungo wa Kenya na Southampton, aliiibukia akademi ya JMJ ya kwao mwaka 2006 na wakati huo huo akawa anaazimwa kuchezea Nairobi City Stars.
    Akiwa kijana mdogo chini ya umri wa miaka 15, akasajiliwa AFC Leopards kabla ya kwenda Helsingborg ya Sweden mwaka 2007 kuanza safari ya mafanikio Ulaya iliyomfikisha England sasa baada ya kupitia Scotland.
     
    Ni kama hivyo, yaani wachezaji wa ukanda wetu huku ukiona wanafanya vizuri Ulaya, basi jua hawajaathirika sana na malezi ya huku kwetu, walikwenda kuwahiwa kufundishwa soka kiprofesheno.
    Ukweli ni kwamba wachezaji wetu Afrika Mashariki na Kati wana mapungufu makubwa na hayo ndiyo yanawatofautisha sana na wenzao wa kanda nyingine, hata kimafanikio.
    Vipaji si tatizo – kwani wengi wanaotembelea huku kwetu huvutiwa na vipaji vya vijana wetu kabla ya kuanza kutoa kasoro.
    Msimu huu katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara tunajionea tofauti ya wachezaji wa ukanda wetu na kanda nyingine, kufuatia ujio wa Wazimbabwe wawili, kiungo Thabani Kamsuoko na mshambuliaji Donald Ngoma.  
    Wawili hao wote wapo katika msimu wao wa kwanza Yanga SC baada ya kusajiliwa kutoka FC Platinums ya kwao, Zimbabwe, Ngoma hadi sasa akiwa amecheza mechi 45 na kufunga mabao 24 na  Kamusoko akiwa amecheza mechi 46 na kufunga mabao tisa.
    Tukio la kukumbukwa la utovu wa nidhamu kwa Wazimbabwe hao ni kadi nyekundu aliyopewa Ngoma katika mechi yake ya tatu tangu ajiunge na Yanga kwenye Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati dhidi ya Gor Mahia.
    Ilikuwa ni kadi ambayo ilitokana na Ngoma kurudishia pigo kwa beki wa Gor aliyemchezea rafu na tangu hapo mchezaji huyo hajapata tena adhabu ya kadi ya kumtoa uwanjani.
    Wachezaji wa Tanzania wana michezo ya kifedhuli ya kukera yenye kutia hasira za kuzalisha maamuzi ya kujutia, lakini Ngoma ameweza kuvumilia na sasa anawaponza wao wazigharimu timu zao kwa penalti na pia kutolewa wenyewe kwa kadi.
    Lakini hilo kubwa sana, wachezaji hao wawili kwa kweli kwa sasa ni msaada mkubwa kwa Yanga – wanaibeba mno timu yao katika mashindano yote.
    Ni nadra kukosekana uwanjani, na ikitokea hawapo kuna sababu ambayo kila mmoja ataikubali mara moja.
    Nidhamu yao ni ya hali ya juu siku kuanzia ndani hadi nje ya Uwanja. Wanaishi na wachezaji wenzao vizuri hawana mambo ya kifedhuli hata mbele ya mashabiki wa timu pinzani.
    Kwa kifupi ni wachezaji ambao wanajitambua sana. Hawana maringo pamoja na kwamba wameziteka nafasi za mashabiki na wanaisaidia timu.
     Wanatazama mikataba yao inasemaje, wanaitekeleza ipasavyo. Na hata pale ambapo klabu inapindisha kidogo yaliyomo kwenye kandarasi, huwezi kujua, kwa sababu wawili hao si watu wa malalamiko, ni watu wa kazi.
    Imefikia wakati najiuliza maswali mengi kuhusu wachezaji hao – hivi kwa mchango na umuhimu wao ndani ya Yanga kama wangekuwa wachezaji wa Kitanzania au nchi jirani za Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda ingekuwaje?
    Kamusoko na Ngoma wakipewa ruhusa ya kwenda kwao kwa mapumziko, wanarudi kwa wakati.
    Hivi karibuni Ngoma alipata msiba kwao Zimbabwe, alikwenda kuzika na kurudi mara moja. Alikosekana kwenye mchezo mmoja tu. Ingekuwa akina fulani ingekuwaje. Siyo ndiyo angekuwa kamaliza msimu kwa machungu ya kufiwa na ndugu?
    Ni wachezaji tofauti sana Kamukoso na Ngoma na kama kuna mambo wanaiga kwa wachezaji wenzao wa hapa basi ni mazuri tu.
    Hata wawapo uwanjani, wako tofauti sana haswa inapotokea mechi ngumu, utaona namna ambavyo wanajitahidi kuzungumza na wachezaji wenzao kuweka mikakati ya kuurahisisha mchezo.
    Ni tofauti hata kiuchezaji Kamusoko na Ngoma wanacheza mpira kama wachezaji ambo walifundishwa tangu wakiwa katika umri mdogo. Wanacheza soka ya kitabuni, yaani kufundishwa.
    Wengi wanajua soka ya kitabuni ni kupiga pasi nyingi hata zisizo na manufaa, la hasha – soka ya kitabuni ni ya mipango na malengo.
    Si malaika wao, wanakosea – lakini hata wakikosea unaweza ukahisi nawe pia umekosea. Kwa ujumla, vijana hawa wawili ni mfano wa kuigwa kwa wachezaji wengine wote wanaocheza Ligi Kuu yetu.
    Kwa sababu kwa umuhimu wao pale Yanga, kama wangekuwa akina fulani tuliowazoea mbona tungekoma na hizo kesi, za kachelewa kurudi, kagoma na kadhalika.    
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAMUSOKO NA NGOMA WANGEKUWA AKINA FULANI, MBONA TUNGEKOMA! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top