• HABARI MPYA

  Jumanne, Mei 24, 2016

  NIYONZIMA: TUKO TAYARI KWA TIMU YOYOTE TUTAKAYOPANGWA NAYO

  Na Somoe Ng’itu, DAR ES SALAAM
  KIUNGO wa Yanga SC, Haruna Niyonzima amesema kwamba hawana wasiwasi na timu yoyote watakayopangiwa nayo katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
  Droo ya mashindano yote, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika zinapangwa leo makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mjini Cairo, Misri kuanzia Saa 6:30 mchana.
  Na Niyonzima amesema kwamba Yanga sasa ni timu ambayo wachezaji wake wana uzoefu wa kutosha wa mashindano makubwa baada ya kucheza mfululizo.
  Haruna Niyonzima (katikati) amesema hawaihofii timu yoyote watakayopangwa nayo hatua ya makundi Kombe la Shirikisho

  “Katika kipindi cha miaka hii mitatu tumecheza na timu za Kaskazini mwa Afrika, Kusini na huku kwetu Mashariki, bahati mbaya hatujakutana na timu za Magharibi ambazo kwa sasa si tishio,”amesema Niyonzima.
  Nahodha huyo wa Amavubi amesema kwamba katika kundi lolote watakaloangukia watapambana wafanye vizuri ili wafike mbali.
  Mbali na Yanga, timu nyingine zilizoingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho ni mabingwa watetezi, Etoile du Sahel ya Tunisia, Ahly Tripoli ya Libya, MO Bejaia ya Algeria, Medeama ya Ghana, FUS Rabat, Kawkab zote za Morocco na TP Mazembe ya DRC.
  Katika Ligi ya Mabingwa Afrika kuna Al Ahly, Zamalek zote za Misri, AS Vita ya DRC, ASEC Mimosas ya Ivory Coast, ES Setif ya Algeria, Enyimba ya Nigeria, Wydad Athletic Club ya Morocco na Zesco ya Zambia.
  (Somoe Ng'itu ni mwandishi wa gazeti la Nipsahe)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NIYONZIMA: TUKO TAYARI KWA TIMU YOYOTE TUTAKAYOPANGWA NAYO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top