• HABARI MPYA

  Saturday, May 28, 2016

  YANGA ‘YAWATIA PINGU’ HADI 2019, BARTHEZ, YONDAN NA OSCAR JOSHUA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC haitaacha mchezaji yeyote mzawa katika kikosi chake cha sasa na nyota waliomaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu wameongezewa miaka miwili kila mmoja.
  Nyota ambao sasa wataitumia Yanga hadi mwaka 2019, ni pamoja na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Oscar Joshua, Pato Ngonyani, Kevin Yondan na Juma Abdul.
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE inafahamu kwamba wote hao walisani mapema mwezi huu katika kipindi ambacho, Yanga ilisaini pia wachezaji wapya, beki Hassan Kessy kutoka Simba na kiungo Juma Mahadhi kutoka Coastal Union.
  Lakini pamoja na kutokuwa na mpango wa kuacha mchezaji mzawa, Yanga inaendelea kufanya tathmini ya wachezaji wake wa kigeni, kama inaweza kumuacha angalau mmoja isajili mpya wa kuongeza nguvu katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
  Oscar Joshua ameongeza Mkataba mpya wa miaka miwili Yanga SC

  Na mchezaji aliye katika hatari ya kuachwa ni kiungo Issoufou Boubacar aliyesajiliwa dirisha dogo kutoka Niger, lakini bado hajamshawishi kiasi cha kutosha kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm.
  Pamoja na kufunga bao katika sare ya 1-1 na Al Ahly ya Misri katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa, Dar es Salaam, Boubacar bado hajaonekana kama mchezaji muhimu Yanga.
  Na ikitokea mchezaji mpya wa kigeni kutaka kusajiliwa Yanga, basi kiungo huyo wa pembeni anaweza kuwa wa kwanza kufikiriwa kuachwa.
  Yanga imemaliza msimu vizuri ikitwaa mataji yote matatu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC).
  Juma Mahadhi (katikati) akisaini Yanga kutoka Coastal Union
  Yanga pia imefanikiwa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola katika mchujo wa kuwania hatua hiyo kwa jumla ya mabao 2-1, ikkishinda 2-0 Dar es Salaam na 1-0 Dundo.
  Yanga iliangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho, baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 2-1 Alexandria.
  Katika Ligi ya Mabingwa, Yanga ilianza vizuri tu kwa kuzitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani kabla ya kuitoa na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Kigali na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
  Na kikosi cha Yanga msimu huu kilikuwa; Makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Benedicto Tinocco na Deo Munishi ‘Dida’.
  Mabeki; Juma Abdul, Mwinyi Haji, Oscar Joshua, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Pato Ngonyani na Nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro'.
  Viungo; Thabani Kamusoko, Salum Telela, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Said Juma, Issoufou Boubacar, Deus Kaseke na Godfrey Mwashiuya.
  Washambuliaji; Donald Ngoma, Matheo Anthony, Amissi Tambwe, Malimi Busungu na Paul Nonga.
  Benchi la ufundi la Yanga liko chini ya Kocha Mkuu Mholanzi, Hans van der Pluijm, Kocha Msaidizi; Juma Mwambusi, Kocha wa makipa; Juma Pondamali, Daktari; Edward Bavu, Mchua Misuli; Jacob Onyango, Mtunza Vifaa; Mohammed Mpogolo na Meneja; Hafidh Saleh.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA ‘YAWATIA PINGU’ HADI 2019, BARTHEZ, YONDAN NA OSCAR JOSHUA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top