• HABARI MPYA

  Thursday, May 26, 2016

  KIIZA ALALAMIKA KUDHULUMIWA UFUNGAJI BORA KOMBE LA ASFC

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa Simba SC, Hamisi Friday Kiiza amesema kwamba yeye ndiye mfungaji bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) 2016.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo, mshambuliaji huyo wa Uganda amesema kwamba alishangaa jana TFF kumtaja mchezaji wa Ndanda FC, Atupele Green Jackson ndiye mfungaji bora.
  “Nimeshangaa sana, mimi ndiye mfungaji bora, nimefunga mabao matano jumla katika mashindano haya hadi tunatolewa Robo Fainali,”amesema Kiiza.
  Mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Kiiza amelalamikia kudhulumiwa ufungaji bora wa Kombe la ASFC

  Mchezaji huyo wa zamani wa Yanga, amesema alifunga mabao mawili katika mechi dhidi ya Burkina Fasso mjini Morogoro na mawili mengine dhidi ya Singida United na moja dhidi ya Coastal Union, yote Dar es Salaam.
  Akizungumzia madai ya Kiiza, Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Jemadari Said Kazumari amesema kwamba kwa mujibu wa rekodi walizonazo, Atupele ndiye aliyefunga mabao mengi.
  “Kwa mujibu wa rekodi zetu, Atupele ndiye mfungaji bora, tena si kwa tu kufunga mabao mengi kwenye mashindano, hata kufunga mabao mengi katika mechi moja. Ndiye mchezaji aliyefunga mabao manne kwenye mechi moja,”amesema Jemadari.
  Michuano ya Kombe la TFF ASFC jana imefikia tamati kwa Yanga kutwaa ubingwa, ikiifunga Azam FC mabao 3-1 katika fainali Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Aidha, mbali na Atupele kutangazwa mfungaji bora jana, kipa wa Azam FC, Aishi Manula ameshinda tuzo ya mlinda mlango bora na beki wa Yanga, Juma Abdul ndiye mchezaji bora wa mashindano.
  Atupele Jackson baada ya kukabidhiwa tuzo yake ya mfungaji bora wa Kombe la ASFC jana
      

  Kiiza mbali na kuikosa tuzo ya ufungaji bora wa Kombe la ASFC, pia alizidiwa kete na mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe katika ufungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Kiiza amemaliza na mabao 19, ingawa hakucheza mechi mbili za mwisho baada ya kutofautiana na uongozi wa Simba, wakati Tambwe alimaliza na mabao 21.
  Tayari Kiiza ameamua kuachana na Simba SC baada ya msimu kutokana na tofauti zake na uongozi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KIIZA ALALAMIKA KUDHULUMIWA UFUNGAJI BORA KOMBE LA ASFC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top