• HABARI MPYA

  Monday, May 30, 2016

  KIPRE TCHETCHE ‘ATIKISA KIBERITI’ AZAM, ASEMA ANATAKA KUONDOKA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI Muivory Coast wa Azam FC, Kipre Herman Tchetche (pichani kushoto) amesema kwamba inatosha sasa kucheza Tanzania na anahitaji kwenda kupata changamoto nyingine sehemu nyingine.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE jana kutoka kwao, Ivory Coast, Kipre amesema kwamba anataka kuzungumza na uongozi wa Azam FC umruhusu kuondoka.
  “Inatosha kwa muda ambao nimecheza Tanzania, nahitaji kuondoka kwenda kutafuta changamoto nyingine kwingine. Nimekuwa na maisha mazuri sana Azam, viongozi na wamiliki wanajali sana wachezaji, lakini nalazimika kuyaacha yote,”amesema.
  Tchetche amesema kwamba hana mpango wa kuhamia klabu nyingine ya Tanzania na habari za yeye kuwa na mpango wa kwenda kwa mahasimu, Yanga ni uzushi.
  “Nitoke Azam, niende Yanga? Usinifanye nicheke, mimi nimesema sitaki kuendelea kucheza Tanzania na hadi sasa sijasaini kokote hadi nipewe ruhusa na uongozi wa Azam,”amesema.
  Kipre Tchetche (kushoto) akiwa na pacha wake, Kipre Michael Balou ambaye wanacheza naye Azam FC 

  Kipre ambaye amebakiza mwaka mmoja katika Mkataba wake, amesema kwa sasa yupo mapumzikoni kwao Ivory Coast na anatarajia kuwasiliana na uongozi wa Azam juu ya mpango wake huo.
  Wakati Kipre akisema hivyo, habari zisizo rasmi zinasema mchezaji huyo tayari amesaini klabu moja ya Uarabuni.
  Kuhusu hilo, Kipre amesema; “Sijasaini popote, nimesema tu sitaki kuendelea kucheza Tanzania,”.
  Wazi klabu itakayothubutu kumsaini Kipre Tchetche itakuwa ‘imeliwa’ kwa sababu mchezaji huyo ana Mkataba na Azam ambao mwenyewe anakiri.
  Lakini kwa wenye uzoefu na mchezaji huyo tangu amejiunga na Azam FC mwaka 2011 wanasema Kipre anatikisa kiberiti ili apatiwe fedha na kuongezwa Mkataba.
  “Mwaka juzi pia alifanya hivyo, alikwenda sijui Malaysia, akataka kusaini, uongozi ukamrudisha hapa na kumuongezea Mkataba mnono na kumpa fedha nyingi. Sasa kwa kuwa amebakiza mwaka mmoja tena, anataka Mkataba mpya kwa staili ile ile,”kimesema chanzo kutoka Azam FC.
  Habari zaidi zinasema kufuatia hofu ya mchezaji huyo kusaini Uarabuni, Azam FC imetuma angalizo Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) juu ya suala hilo.
  Hii maana yake klabu itakayomsaini, au iliyomsaini Kipre Tchetche haitaidhinishiwa mchezaji huyo  na FIFA – hadi Azam FC itoe ridhaa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KIPRE TCHETCHE ‘ATIKISA KIBERITI’ AZAM, ASEMA ANATAKA KUONDOKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top