• HABARI MPYA

  Alhamisi, Mei 26, 2016

  TFF YAWACHOMOLEA CECAFA KUANDAA KOMBE LA KAGAME

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  TANZANIA imejitoa kuandaa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame mwaka 2016.
  Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema mapema leo kwamba kujitoa kwako kumetokana na kubanwa na ratiba za mashindano mbalimbali ya kimataifa kati ya Juni na Septemba.
  “Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania halitaandaa mashindano ya CECAFA Kagame cup 2016. Hii ni kutokana na muingiliano wa ratiba ya kimataifa,”amesema Malinzi katika taarifa yake fupi kwa Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini leo.


  Mabingwa Azam walimpelekea Ikuku, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete Kombe la Kagame mwaka jana. Pichani Nahodha Msaidizi, Himid Mao anamkabidhi taji hilo 

  TFF ililikubalia Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kuandaa kwa mara ya pili michuano ya Kombe la Kagame mwaka huu, baada ya mwaka jana kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.
  Katika mashindano ya mwaka jana, Azam FC waliibuka mabingwa baada ya kuifunga Gor Mahia ya Kenya katika fainali 2-0, mabao ya Nahodha, John Bocco dakika ya 17 na Kipre Herman Tchetche dakika ya 64 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Na inaonekana wazi TFF imamua kuachana na Kombe la Kagame, baada ya timu yenye mvuto zaidi wa mashabiki nchini, Yanga SC kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika hivyo haitaweza kushiriki michuano hiyo ya CECAFA.
  Na inaonekana TFF inaona inahofia kupata hasara kufanya mashindano hayo bila ya Yanga kushiriki – wakati huo huo inaonekana pia timu nyingine yenye mashabiki wengi nchini, Simba SC haiko tayari.
  Yanga ambao ni mabingwa wa mataji yote matatu nchini msimu huu, Ngao ya Jamii, Kombe la Ligi na Kombe la TFF maarufu kama ASFC, imepangwa Kundi A katika Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na mabingwa wa zamani barani, TP Mazembe ya DRC, MO Bejaia ya Algeria na Medeama ya Ghana.

  Winga machachari wa Azam FC, Farid Mussa Malik akiruka na mpira wake kwanja la beki wa Gor Mahia, Harun Shakava katika mchezo wa fainali ya Kagame Agosti 2, mwaka jana Uwanja wa Taifa

  Kundi B linaundwa na timu za Kaskazini mwa Afrika tupu ambazo ni Etoile du Sahel ya Tunisia ambao ni mabingwa watetezi, Ahly Tripoli ya Libya, FUS Rabat na Kawkab zote za Morocco.
  Yanga watafungua dimba na Mouloudia Olympique Bejaia nchini Algeria Juni 17, mwaka huu katika Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika.
  Siku hiyo, mabingwa wa zamani wa Afrika, TP Mazembe ya DRC watakuwa wenyeji wa Medeama ya Ghana katika mchezo mwingine wa kundi hilo.
  Mechi za Kundi B siku hiyo; Kawkab Marakech watakuwa wenyeji wa mabingwa watetezi Etoile du Sahel katika mchezo wa Kundi B nchini Morocco, wakati F.U.S Rabat watakuwa wenyeji wa Ahly Tripoli nchini Morocco pia.
  Ikitoka Algeria, Yanga itarejea nyumbani kuikaribisha TP Mazembe Juni 28, kabla ya kumaliza na Medeama ya Ghana Julai 15, Dar es Salaam pia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TFF YAWACHOMOLEA CECAFA KUANDAA KOMBE LA KAGAME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top