• HABARI MPYA

  Jumapili, Mei 29, 2016

  HARAMBEE WABANWA NYUMBANI SARE 1-1 NA TAIFA STARS KASARANI

  Na Mwandishi Wetu, NAIROBI
  TANZANIA ‘Taifa Stars’ imelazimisha sare ya 1-1 na wenyeji Kenya ‘Harambee Stars’ katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa jioni ya leo Uwanja wa Kasarani, Nairobi, Kenya.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa wa Uganda, Brian Nsubuga aliyesaidiwa na Bugembe Hussein na Katenya Ronald, Stars ya kocha Charles Boniface Mkwasa iliibana Kenya na kutangulia kupata bao.
  Licha ya kuongozwa na kiungo wa Southampton ya Ligi Kuu ya England, Victor Wanyama lakini Harambee Stars walijikuta katika wakati mgumu mbele ya Taifa Stars na mwishowe wakapata sare nyumbani.   
  Kiungo Jonas Mkude alimdhibiti vizuri Wanyama katikati ya Uwanja na akashindwa kufurukuta hadi alipofunga kwa penalti. 
  Elias Maguli amefunga bao la Taifa Stars leo dhidi ya Harambee Stars mjini Nairobi 

  Taifa Stars iliyotumia kikosi cha pili, ilianza kupata bao dakika ya 32 kupitia kwa mshambuliaji wa Stand United, Elias Maguli aliyemalizia kwa kichwa krosi ya beki wa kulia Juma Abdul.
  Refa akawapa penalti ya utata Kenya baada ya Ayoub Timbe kuangushwa na kiungo Deus Kaseke – na Wanyama akaenda kufunga dakika ya 38 kwa mkwaju ‘usio wa kiufundi’ ambao kipa Deo Munishi ‘Dida’ alikaribia kuuokoa baada ya kuufuata vizuri, lakini ukamzidi kasi.
  Kipindi cha pili, Kenya waliamua kucheza kwa kujihami zaidi kuepuka aibu ya kufungwa nyumbani na mchezo ukaisha kama walivyotaka wenyeji kwa sare ya 1-1.
  Kocha wa Kenya, Stanley Okumbi alionekana kufurahia katika benchi lake baada ya filimbi ya mwisho, wakati Mkwasa alionekana kutofurahia matokeo.
  Kikosi cha Kenya; Boniface Oluoch, Joakins Atudo, Abud Khamis, Eugene Asike, David Owino, Anthony Akumu/Ally Abondo dk78, Victor Wanyama, Ayub Timbe/John Makwatta, Humphrey Mieno/ Cliford Miheso dk56, Eric Yohanna na Jesse Were/Wycliff Ochomo dk70.
  Tanzania; Deo Munishi ‘Dida’/Aishi Manula dk62, Juma Abdul, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Jonas Mkude/Mohammed ‘Mo’ Ibrahim dk62, Himid Mao, Shiza Kichuya, Mwinyi Kazimoto, Elias Maguli/Jeremiah Juma dk83 na Deus Kaseke/Farid Mussa dk65.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HARAMBEE WABANWA NYUMBANI SARE 1-1 NA TAIFA STARS KASARANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top