• HABARI MPYA

  Sunday, May 29, 2016

  NI REAL MADRID ‘WAFALME’ ULAYA, ATLETICO AFA KWA MATUTA SAN SIRO

  REAL Madrid wametwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa ushindi wa penalti 5-3 baada ya sare ya 1-1 dhidi ya mahasimu wao, Atletico Madrid usiku huu Uwanja wa San Siro, Milan, Itali.
  Kipa Keilor Navas Gamboa alijitanua vizuri langoni na Juan Francisco Torres Belen ‘Juanfarn’ akaona lango dogo na kugongesha nguzo ya pembeni penalti ya nne ya Atletico.
  Cristiano Ronaldo akaenda kwa kujiamini kupiga penalti ya mwisho ya Real Madrid na kumtungua kipa Jan Oblak wa Atletico kuwapa Magalactiico taji la 11 la Ligi ya Mabingwa.
  Wengine waliofungaa penalti za Real Madrid ni Lucas Vazquez, Marcelo, Gareth Bale na Sergio Ramos, wakati Atletico zimefungwa na  Antonio. Griezmann, Gabi na Saul.
  Nahodha wa Reald Madrid, Sergio Ramos akiinua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuifunga Atletico Madrid kwa penalti 5-3 usiku huu Uwanja wa San Siro PICHA ZAIDI GONGA HAPA   

  Mchezo huo uliochezeshwa na marefa wa England, Mark Clattenburg aliyesaidiwa na Simon Beck na Jake Collin, Real Madrid walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa beki wake na Nahodha, Sergio Ramos dakika ya 15 aliyemalizia mpira wa kichwa wa winga Gareth Bale.
  Baada ya bao hilo, Real waliuteka mchezo na kupeleka mashambulizi mengi langoni mwa Atletico, lakini bahati haikuwa yao.
  Kipindi cha pili, kocha Diego Simeone wa Atletico alianza na mabadiliko, akimpumzisha kiungo Muargentina mwenzake Augusto Matias Fernandez na kumuingiza kiungo Mbelgiji Yannick Ferreira Carrasco.
  Mabadiliko hayo yalikuwa msaada kwa kikosi cha Simeone, kwani ni Carrasco aliyekwenda kuisawazishia Atletico dakika ya 79, akimalizia pasi ya Juan Francisco Torres Belen, maarufu kama Juanfran.
  Bao hilo ‘likauamsha’ upya mchezo huo, timu zote zikicheza ka nguvu na kasi kusaka bao la ushindi, lakini dakika 90 zikamalizika kwa sare ya 1-1.
  Awali ya hapo, mshambuliaji hatari wa Atletico Madrid, Antonio Griezmann alipaisha mkwaju wa penalti dakika ya 48 baada ya Fernando Torres kuangushwa na Pepe kwenye boksi.
  Kocha Mfaransa, Zinadine Zidane aliwapumzisha Karim Benzema, Daniel Carvajal na Toni Kroos kipindi cha pili na kuwaingiza Isco, Danilo na Lucas Vazquez.
  Katika dakika 30 za nyongeza timu zote zilicheza kwa tahadhari mno na mwishoni mwa mchezo, Simeone akawatoa Filipe Luis na Koke na kuwaingiza Lucas Hernandez na Thomas Teye Partey.
  Na baada ya kushinda kwa penalti 5-3, Real inafikisha mataji 11 ya Ligi ya Mabingwa, mengine ikitwaa misimu ya 1955–1956, 1956–1957, 1957–1958, 1958–1959, 1959–1960, 1965–1966, 1997–1998, 1999–2000, 2001–2002 na 2013–2014.
  Kikosi cha Real Madrid kilikuwa; K. Navas, Sergio Ramos, Pepe, Marcelo, Daniel Carvajal/Danilo dk52, L. Modric, G. Bale, T. Kroos/ Isco dk72, Casemiro, Cristiano Ronaldo na K. Benzema/Lucas Vazquez dk77.
  Atletico Madrid; J. Oblak, Juanfran, Filipe Luis/ L. Hernandez dk109, D. Godín, S. Savic, Gabi, A. Fernández/Y. Carrasco dk46, Saul, Koke/T. Partey dk116, Fernando Torres na A. Griezmann.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NI REAL MADRID ‘WAFALME’ ULAYA, ATLETICO AFA KWA MATUTA SAN SIRO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top