• HABARI MPYA

    Sunday, May 10, 2015

    MSUVA AWAOMBA YANGA SC WAMUUZE ‘BEI POA’ AFRIKA KUSINI

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    MFUNGAJI bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simon Msuva ameomba klabu yake Yanga SC iwatajie ‘bei rahisi’ Bidvest Wits ya Afrika Kusini ili waweze kumnunua.
    Msuva amerejea jana jioni Dar es Salaam baada ya siku tatu za kuwa Afrika Kusini kwa mipango ya kujiunga na klabu hiyo ya Ligi Kuu nchini humo.  
    “Namshukuru Mungu mipango imekwenda vizuri huko nilipokuwa, nimerudi hapa nawaachia sasa Bidvest waanze mazungumzo na Yanga. Sitarajii kama watatajiwa bei kubwa,”amesema. 
    BIN ZUBEIRY inafahamu Bidvest Wits wameridhika na uwezo Msuva na sasa wanataka kufungua majadiliano na klabu yake, Yanga SC. 
    Simon Msuva ameomba Yanga SC isiwatajie bei kubwa Bidvest Wits wakileta ofa 

    Msuva amebakiza mwaka mmoja katika Mkataba wake Yanga SC na Wits iko tayari kutumia si zaidi ya dola za Kimarekani 100,000 (Sh. Milioni 200) kukamilisha dili zima la mchezaji huyo- kwa maana ya malipo ya mchezaji kusaini na ada ya uhamisho kwa klabu yake.  
    Msuva aliondoka Dar es Salaam Jumatano wiki hii akiwa tayari ameipa Yanga SC ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, huku pia akiwa anaongoza kwa mabao, 17 akifuatiwa na mchezaji mwenzake wa timu hiyo, Amissi Tambwe mabao 14.   Amekosa mechi mbili za mwisho dhidi ya Azam FC Yanga ikilala 2-1 na jana dhidi ya Ndanda ya Mtwara timu yake ikifungwa pia 1-0.
    Tangu ajiunge na Yanga SC mwaka 2012 akitokea Moro United, Msuva ameifungia timu hiyo mabao 35 jumla katika mechi 102 za mashindano yote.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MSUVA AWAOMBA YANGA SC WAMUUZE ‘BEI POA’ AFRIKA KUSINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top