• HABARI MPYA

  Jumanne, Mei 19, 2015

  NOOIJ AMRUDISHA NYUMBANI KIUNGO WA YANGA BAADA YA STARS KULALA 1-0 JANA

  Na Mahmoud Zubeiry, RUSTENBURG
  KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mholanzi Mart Nooij amemrejesha nyumbani kiungo Said Juma ‘Makapu’, (pichani kulia) siku moja baada ya timu hiyo kupoteza mchezo wa kwanza Kombe la COSAFA.
  Makapu ameondoka leo kwa gari ndogo mjini hapa kwenda Johannesburg, kupanda ndege kurejea Dar es Salaam.
  Kiungo huyo wa mabingwa wa Tanzania, Yanga SC ameshindwa kuichezea Taifa Stars katika Kombe la COSAFA kutokana na maumivu ya mgongo.
  Makapu hakuweza kabisa kufanya mazoezi na Taifa Stars tangu afike hapa wiki iliyopita, kutokana na maumivu aliyoyapata katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ndanda FC mjini Mtwara mwanzoni mwa mwezi.
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto amesema kwamba mchezaji anarejea leo nyumbani kwa ajili ya vipimo zaidi na matibabu.
  Stars jana imefungwa bao 1-0 na Swaziland katika mchezo wa kwanza wa Kundi B Kombe la COSAFA Uwanja wa Royal Bafokeng Sports Palace mjini hapa.
  Matokeo hayo yanaiweka Stars katika mazingira magumu ya kwenda Robo Fainali- baada ya Madagascar kuifunga 2-1 Lesotho katika mchezo wa kwanza.
  Mrisho Ngassa akimtoka beki wa Swaziland katika mchezo wa jana ambao Taifa Stars ililala 1-0

  Stars sasa lazima ishinde mechi zake mbili zijazo dhidi ya Lesotho na Madagascar ili kuangalia uwezekano wa kwenda Robo Fainali.
  Swaziland ambayo bao lake pekee lilifungwa na  Sifiso Mabila kwa shuti kali dakika ya 42 baada ya kutanguliziwa pasi kwenye njia na Xolani Sibandze aliyemtoka Oscar Joshua upande wa kushoto, waliizidi ufundi uwanjani Stars jana.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NOOIJ AMRUDISHA NYUMBANI KIUNGO WA YANGA BAADA YA STARS KULALA 1-0 JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top