• HABARI MPYA

    Wednesday, May 27, 2015

    MBWANA SAMATTA HAKUTAKA ‘KUJIRUSHA AKILI’, ILA MESSI…

    KATIKATI ya Juni mwaka juzi, nilifanya mahojiano na mshambuliaji Mbwana Ally Samatta tukiwa kwenye ndege tunarejea kutoka Morocco.
    Taifa Stars, timu ya taifa ya Tanzania ilikuwa inatokea mjini Marakech kucheza mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia mwaka jana Brazil dhidi yaa wenyeji, Morocco.
    Tanzania ilicheza mpira mzuri chini ya kocha Mdenmark, Kim Poulsen na kufungwa mabao 2-1 kwa taabu Uwanja wa Marakech Juni 8, mwaka juzi. 
    Nakumbuka siku hiyo, bao pekee la Tanzania lilifungwa na kiungo rasta, Amri Ramadhani Kiemba dakika ya 61, huku mabao ya wenyeji yakifungwa na Abderrazak Hamdallah kwa penalti dakika ya 39 na Youssef El-Arabi dakika ya 51.
    Katika mahojiano yangu na Mbwana Samatta aliyekuwa mwiba wa safu ya ulinzi ya Morocco siku hiyo, alisema kwamba anajuta kusaini Mkataba wa muda mrefu (miaka minne) na klabu yake, TP Mazembe ya DRC.
    Samatta alisema kwamba Mkataba huo ulifikia wakati unambana kwa maana zote- hawezi kuondoka na pia maslahi anayopata hayaendani na kiwango chake.
    Lakini pamoja na yote, Samatta akasema hana namna zaidi ya kuvumilia hadi Mkataba wake uishe au kuomba Mazembe imuuze, ili akasaini Mkataba mwingine ambao utazingatia thamani yake ya wakati husika.
    Samatta alijiunga na Mazembe akitokea Simba SC wakati mchezaji mdogo tu- lakini baada ya kuanza kazi Lubumbashi, kiwango chake kikakuwa na kutengeneza jina na kukuza thamani yake pia.
    Baadaye anakuja kugundua kuna wachezaji hawafikii uwezo wake, lakini wanalipwa fedha nyingi Ulaya na sehemu nyingine hapa Afrila, au Asia na Amerika.
    Na akasema wazi hiyo inamuumiza sana na angetamani siku zirudi nyuma, Mkataba wake na Mazembe usainiwe upya. Lakini wapi, wakati umepita na tayari yuko ndani ya pingu ya timu ya Moise Katumbi Chapwe kwa maslahi ambayo hayaendani na uwezo wake.
    Tatizo moja tu, wachezaji wa Tanzania hawana soko nje na Samatta alipopata nafasi ya kwenda Mazembe, timu kubwa Afrika, yeye na washauri wake hawakuona sababu ya kuipoteza nafasi hiyo.
    Mshahara wa Sh. Milioni 5 kutoka chini ya Sh. Milioni 1 aliyokuwa analipwa Simba SC, hakika ilikuwa hatua kubwa sana kwake ya kimafanikio miaka minne iliyopita.   
    Lakini miaka miwili tu baadaye, akagunua inambana- anastahili kulipwa zaidi ya hivyo- tena sana.
    Tatizo ambao alikumbana nalo Samatta ni tatizo la kawaida mno kwa wachezaji wa Tanzania hapa hapa nyumbaji. Wanapokuwa wanaibuka, wanasainishwa Mikataba mirefu kwa maslahi madogo.
    Baadaye wanapokuja kufunguka kifikra na kugundua thamani yao halisi, huwa mtihani kidogo na wakati mwingine huwaathiri hata kisaikolojia na kushindwa kucheza vizuri.
    Hata sababu za wachezaji kuhama hama timu ndani ya timu kubwa, labda kutoka upande hadi mwingine kwa mahasimu wa jadi, Simba na Yanga ni maslahi tu.  
    Wiki hii umeibuka mjadala kuhusu Mkataba wa kiungo mshambuliaji, Ramadhani Singano ‘Messi’ katika klabu ya Simba.
    Mtu aliyejitambulisha Meneja wa Messi anadai Mkataba wa mchezaji wake na klabu umechezewa na kurefushwa, kwani wanavyofahamu wao unapaswa kumalizika mwaka huu.
    Lakini SImba SC wanasema Messi amebakiza mwaka mmoja Msimbazi. Tangu mwishoni mwa mechi za Ligi Kuu msimu huu, Messi alionyesha kiu ya Mkataba mpya.
    Hakuna hakika kama Messi kweli anajua Mkataba wake halisi, ila anataka ‘kujirusha akili’ kushinikiza Mkataba mpya utakaoendana na thamani yake ya sasa, au yuko sahihi katika madai yake kupitia meneja wake.
    Messi ni kijana aliyeshika dini yake ya Kiislamu, anayesali sala tano- akijua kabisa Uislamu unakataza mtu kusema uongo, sidhani anaweza kuthubutu kusema uongo katika hili.
    Lakini pia inawezekana mtu kuamua kujirusha akili ili kusahihisha makosa aliyoyafanya kipindi cha nyuma. Vigumu kumjua mkweli hapa, kwa sababu mimi na wasomaji wangu hatukuwa mashahidi wakati wa kusainiwa Mkataba huo.
    Ila kwa maelezo ya viongozi wa Simba SC ni kwamba nakala ya Mkataba wao na mchezaji huyo iliwasilishwa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) mara tu uliposainiwa.
    Na Simba SC wanasema nakala waliyonayo wao, inafanana na ile ambayo ipo TFF, isipokuwa nakala ya Messi kwanza ni fotokopi na pia kuna seehemu maandishi kama yamepandiana kuashiria ulichezewa.
    Messi naye anasema vile vile, Mkataba wake umechezewa. Yaani Simba SC wameghushi saini hiyo.
    Hii ni kesi rahisi mno kuimua, lakini kiutaalamu. Suala lipelekwe jeshi la Polisi ili uchunguzi ufanyike. Ila kitu ambacho nimejfunza hadi sasa, wachezaji wa Tanzania huamua kujirusha akili ii wapate maslahi bora.
    Sitaki kuamini kama na Messi amefanya hivyo, ila ninachojua Mbwana Samatta hakutaka kujirusha akili, alipogundua makosa yake, bali aliamua kuvumilia amalize Mkataba na kuondoka kwenda kusaini Mkataba utakaoendana na kiwango na thamani yake ya sasa. Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MBWANA SAMATTA HAKUTAKA ‘KUJIRUSHA AKILI’, ILA MESSI… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top