• HABARI MPYA

  Jumapili, Mei 31, 2015

  KWA USAJILI HUU, SIMBA SC WATASUBIRI SANA

  WAKATI nafikiria kuandika makala haya, nilijua kuna watu nitawaudhi. Wasiopenda ukweli. Na nimejitayarisha kwa lawama, matusi na kejeli- tu kwa maslahi ya Simba SC na soka ya Tanzania kwa ujumla.
  Baada ya kumalizika kwa msimu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, klabu mbalimbali zimeingia kwenye mawindo ya usajili wa wachezaji wapya.
  Kama kawaida, macho na masikio ya wengi yanategwa kwa usajili wa vigogo, Simba na Yanga SC, ambao ni wapinzani wa jadi.
  Hadi sasa, Simba SC imekwishasajili wachezaji wapya watano ambao ni kipa Mohammed Abraham kutoka JKU ya Zanzibar, mabeki Samih Hajji Nuhu kutoka Azam FC, Mohammed Fakhi wa JKT Ruvu, kiungo Peter Mwalyanzi wa Mbeya City na mshambuliaji Mussa Hassan Mgosi kutoka Mtibwa Sugar.
  Yanga nao wamesajili wachezaji wane, kipa Benedictor Tinocco kutoka Kagera Sugar, beki Mwinyi Hajji Mngwali kutoka KMKM na viungo washambuliaji, Deus Kaseke kutoka Mbeya City na Malimi Busungu kutoka Mgambo JKT. 
  Ukitazama wachezaji ambao wamesajiliwa na Yanga SC hadi sasa, utaona ni ambao walikuwa wanahitajika baada ya tathmini ya kikosi cha timu hiyo msimu uliopita.
  Ikiwa tayari ina makipa wawili wazoefu, Ally Mustafa ‘Barthez’ na Deo Munishi ‘Dida’- Yanga imesajili kipa chipukizi, kijana mdogo mwenye umbo zuri na kipaji. Tinocco.
  Watu wengi wamekuwa wakipigia kelele beki ya kushoto ya Yanga SC msimu huu ilikuwa dhaifu- hawaridhishwi na uchezaji wa Oscar Joshua wakati huo huo chipukizi aliyesajiliwa msimu uliopita, Edward Charles majeruhi yalimrudisha nyuma.
  Hilo ndilo jibu kwa nini Mwinyi Hajji Mngwali amesajiliwa Yanga SC- beki wa KMKM ambaye tayari yupo timu ya taifa, Taifa Stars.
  Kiungo mshambuliaji Mrisho Khalfan Ngassa amehamia Free State Stars ya Afrika Kusini na Andrey Coutinho anaweza kuachwa- hayo ni majibu kwa nini wamesajiliwa Busungu na Kaseke.
  Kaseke na Busungu wote ni wazoefu katika Ligi Kuu, ambao sasa wanaingia Yanga SC kujipambanua zaidi kisoka.
  Haya twende Simba SC; kwanza aina ya wachezaji wote ambao wamesajiliwa hadi sasa ni wa kawaida mno, wakati timu inahitaji wachezaji bora zaidi ili kurejesha makali yake.
  Msimu wa tatu umemalizika Simba SC hawamo ndani ya mbili bora na maana yake hawana nafasi ya kucheza michuano ya Afrika.
  Sababu ni ile ile, kocha wa zamani wa Wekundu hao wa Msimbazi, Mcroatia Zdravko Logarusic aliwahi kusema; “Hakika ninahitaji wachezaji wenye sifa za kimataifa, nahitaji beki mmoja, kiungo wa ulinzi na mshambuliaji, ili niwaunganishe na nilionao kupata kikosi bora,”alisema Logarusic Julai 16, mwaka jana, Uwanja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) nilipofanya naye mahojiano.
  Hiyo ilikuwa ni baada ya Simba SC kukamilisha usajili wake wa kikosi cha msimu uliopita na kuanza mandalizi ingizo jipya kikosini wakati huo walikuwa vijana kama Peter Manyika, Hussein Sharrif ‘Casillas’, wote makipa, beki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, kiungo Abdi Banda na washambuliaji Mkenya, Paul Kiongera, Ibrahim Hajib na Elias Maguri.   
  Mcroatia huyo akasema kwamba anahitaji wachezaji wapya watatu wa kimataifa katika kikosi chake, beki, kiungo mkabaji na mshambuliaji ili awe na timu bora ya ushindani.
  Na akawazungumzia wachezaji wapya chipukizi waliosajiliwa, akisema kwamba wanatakiwa kujituma ili kufikia kiwango cha kimataifa, kwa sababu Simba SC ni timu kubwa na wao lazima waonyeshe uwezo mkubwa.
  “Wametoka timu ndogo ndogo na wana vipaji, lakini wanatakiwa kufanya bidii hapa, kwa sababu Simba ni timu kubwa, lazima waonyeshe uwezo wa kimataifa,”alisema.
  Kwa bahati mbaya Logarusic akafukuzwa Agosti mwaka jana na timu haikusajili aina ya wachezaji aliowataka kocha huyo, zaidi ya mshambuliaji Emmanuel Okwi aliyetua kwa ngekewa tu.
  Okwi alirejea Simba SC baada ya kujikuta katika mgogoro na iliyokuwa klabu yake, Yanga SC, nadiriki kusema ilikuwa ngekewa- kwa sababu kama si huo mgogoro angebaki Jangwani.
  Patrick Phiri, kocha Mzambia aliyeajiriwa baada ya kufukuzwa Logarusic naye akafukuzwa Desemba, timu ikiwa haina matokeo mazuri.
  Pamoja na kumfukuza Phiri, Simba SC ikafanya usajili mzito kidogo Desemba, ikiwachukua beki Juuko Murushid na washambuliaji Simon Sserunkuma na Dan Sserunkuma kuungana na Waganda wenzao, Joseph Owino na Okwi. 
  Kiongera alitemwa Desemba sababu ya maumivu ya goti, viungo Amri Kiemba na Haroun Chanongo walitolewa kwa mkopo kwa madai walikuwa hawajitumi.
  Mserbia Goran Kopunovic akarithi mikoba ya Phiri na akaanza vyema kwa kuipa timu Kombe la Mapinduzi Janauri.
  Kuingia kwenye Ligi Kuu, Goran amefanikiwa kuifanya Simba SC imalize katika nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na Azam.
  Lakini kwa mwaka wa tatu, mwakani Simba SC hawatacheza michuano ya Afrika, wakiziacha Yanga na Azam ziendelee kuwakilisha nchi.
  Na hawa wachezaji ambao Simba SC inasajili kwa sasa, si aina aina ya wale ambao Logarusic alipendekeza, akapuuzwa na matokeo yake tumejionea. 
  Simba SC ina makipa wanne na wote wazuri, Ivo Mapunda, Hussein Sharrif ‘Casillas’ na wale wadogo Peter Manyika na Dennis Richard.
  Nasikia wanataka kumuacha Casillas kwa sababu haelewani na Ivo- sioni kama ni sahihi, viongozi wa Simba SC wanapaswa kumuelimisha Hussein aweze kuishi na mwenzake vizuri aachane na dhana potofu.  
  Casillas ni kipa mzuri na mzoefu, ambaye akibaki atakuja kuisaidia SImba SC baadaye. Mawazo ya Casillas ni mawazo ya wachezaji wengi a Kitanzania. Na unaanzaje kumshangaa mchezaji mwenye imani za kishirikina wakati klabu zenyewe zinaendekeza ushirikina? 
  Nuhu kweli alikuwa beki chaguo la kwanza Azam FC kabla ya kuumia na kwenda kufanyiwa upasuaji uliomuweka nje misimu miwili. 
  Kwanza aina ya upasuaji aliofanyiwa Nuhu, kuweza tu kurudi kucheza katika kiwango chake ni bahati, lakini pia hajacheza misimu miwili. 
  Sina shaka na uwezo wa Peter Mwalyanzi, lakini sina imani kama anaweza kuchukua namba mbele ya Jonas Mkude, Said Ndemla, Abdi Banda na bado kuna Awadh Juma na Abdallah Seseme ambao wote wanacheza katikati. Wanasema huyu ni kiraka anacheza nafasi nyingi- hapa Simba SC imesajili mchezaji wa akiba anayeweza kuingia kucheza popote. Si vibaya.
  Mohamed Fakhi ni beki mzuri, bwana mdogo- huyu anahitaji muda maana yake anaingia Simba SC kwenda kujiendeleza na baadaye anaweza akawa bora.
  Mgosi ni mkongwe aliyewahi kucheza Simba SC kabla, mzoefu na mfungaji mzuri. Si vibaya kuwa naye kwenye timu, hususan aliyoizoea na anayoipenda.
  Turudi kwenye tatizo la msingi la timu baada ya msimu, wengi walijiridhisha Simba SC kama timu ilikuwa nzuri, ila ilikosa wachezaji wachache muhimu, wenye sifa za kimataifa.
  Na hao wachezaji wenye sifa za kimataifa huwapati kwa ‘shilingi mbili tatu’- lazima utoe fedha ya maana kusajili. SImba SC wanaonekana kama hawako tayari kutoa fedha nyingi kusajili, lakini mwisho wa siku wanatumia fedha nyingi kuliko.
  Mfano tu msimu uliopita, wamesajiliwa Kiongera, Dan Sserunkuma, Simon Sserunkuma wote wachezaji wa kigeni ambao mwisho wa siku hawakuisaidia timu na wanaachwa.
  Labda Simba SC iliwapata kwa bei poa wachezaji hao, lakini je kama wanaondoka baada ya nusu msimu, hii siyo hasara?
  Hapa wana Simba SC hawajasahau kilichotokea kwa wachezaji kama Paschal Ochieng, Daniel Akuffor, Komabil Keita, Lino Musombo na Kanu Mbivayanga.
  Wote hawa walisajiliwa na kuachwa baada ya muda mfupi, tena wengine wakilipwa fedha kibao za kuvunja mikataba yao.
  Wakati umefika Simba SC wajifunze kutokana na makosa na kutokubali kurudia makosa. Huu usajili wa ‘kibakhili’ ndiyo gharama zaidi kwa sababu unasajili mtu ambaye huna uhakika naye, kesho unamuacha na kumlipa.
  Simba SC ifanye mambo kwa uhakika, isajili wachezaji ambao kila mtu akisikia, atakiri Msimbazi sasa kumekucha. Mwenye kununa, anune, mwenye kuchukia achukie, lakini habari ndiyo hiyo, huu usajili ambao wanaufanya Simba kwa sasa ni wa kugombea nafasi ya tatu dhidi ya akina Mbeya City, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar, si wa kugombea ubingwa dhidi ya Yanga na Azam. Alamsiki. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KWA USAJILI HUU, SIMBA SC WATASUBIRI SANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top