• HABARI MPYA

    Wednesday, May 20, 2015

    NOOIJ AMEIPA MTIHANI MZITO TFF, NI JUU YAO KUSUKA, AU KUNYOA

    MAPEMA Agosti mwaka 2010, Rais wa FIFA, Sepp Blatter alizionya timu za Afrika, kama zinataka kushinda Kombe la Dunia basi ziachane na makocha Wazungu na kuamini makocha wao.
    Alisema; “Kocha lazima awe na hisia juu ya wachezaji wake ndani ya nafsi zao na mioyo yao- angalia Nigeria kwa mfano. Wachezaji labda wapo Ulaya, lakini kocha lazima aelewe kwa undani uwezo wao. Vipi mtu anayetoka nje (ya nchi)  anaweza kufanya hivyo?”alihoji.
    Blatter akasema anaamini nchi za Afrika zinaathiriwa pia na maandalizi mabovu.
    Akasema nchi za Afrika zinafanya vizuri katika mashindano ya vijana na Olimpiki, kwa sababu mara nyingi makocha huwa wa nyumbani.
    “Nimekuwa nikiifuatilia soka ya Afrika kwa muda mrefu, kuliko soka ya mabara mengine yote… Wakati zinacheza mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 23, timu za Afrika zinaweza kuwamudu wapinzani wao kutoka sehemu nyingine za dunia,”.
    “Unaweza kusema labda Ulaya hawayapi uzito mashindano ya Olimpiki. Lakini hapana, naweza kukuambia kwamba Ulaya hawafurahii kiwango chao katika mashindano ya Olimpiki. Katika mashindano ya wakubwa, (Vyama vya soka Afrika) haviziandai timu zao vizuri,”.
    “Angalia namna ambavyo timu kutoka sehemu nyingine duniani zinavyojiandaa, fedha wanazotumia na jitihada wanazofanya tayari kushindana. Vyama vya Afrika wakati mwingine vinaajiri kocha kiasi cha mwezi mmoja kabla ya Kombe la Dunia. Hii lazima ikome,” alisema.
    Kwa nini nimekumbuka maneno haya ya Blatter leo, si kwa sababu kwa nini Tanzania haitumii makocha wazawa katika timu zetu, hapana, bali mtihani uliopo mbele ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa sasa juu ya kocha wake, Mholanzi, Mart Nooij. 
    Mwezi ujao tuaanza mechi za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika, lakini tayari Wajumbe wengi wa Kamati ya Utendaji ya TFF wamepoteza imani juu ya Nooij na wanashinikzia aondolewe haraka.
    Nooij ameshinda mechi tatu tu kati ya 14 ambazo ameiongoza Taifa Stars hadi sasa, tano akifungwa na sita akitoa sare. 
    Hasira za Wajumbe wa TFF na Watanzania kwa ujumla zimeongezeka baada ya Taifa Stars kuanza vibaya katika mechi za Kombe la COSAFA kwa kufungwa 1-0 na nchi ambayo wanaamini ni dhaifu, Swaziland.
    Watu wanaongea kwa jaziba hadi mapovu yanawatoka, wanatukana hata wasiostahili. Wanachotaka kocha afukuzwe aletwe kocha mwingine.
    Na nina wasiwasi, iwapo Taifa Stars haitapata matokeo mazuri katika mchezo wake wa pili wa COSAFA leo dhidi ya Madagascar, TFF inaweza kuingia kwenye mtego wa shinikizo la kufukuza kocha.
    Sasa unafukuza kocha zimebaki wiki mbili kabla ya kuanza mechi za kufuzu za AFCON mwaka 2017 nchini Gabon, ambako Tanzania imepangwa Kundi G pamoja na Nigeria, Chad na Misri, nini unatarajia?
    Tutafungua dimba na Misri Juni 13 Cairo na tayari Rais wa TFF, Jamal Malinzi amesema timu itaweka kambi Addis Ababa, Ethiopia baada ya COSAFA.
    Tuna makocha bora hapa Tanzania wenye uwezo wa kufundisha timu ya taifa kwa ufanisi mkubwa, lakini bahati mbaya siku hizi hatuaminiani kwa sababu nyingi tu, nyingine hazina hata maana.
    Tumewahi kufuzu AFCON mara moja tu mwaka 1980 nchini Nigeria na kocha wakati huo alikuwa Joel Bendera, sasa mwanasiasa.
    Bado wanakumbuka enzi zile soka yetu ilikuwa juu, timu ya taifa ikifundishwa na makocha wazawa, mfano Ray Gama (sasa marehemu). Leo nini kimetokea?
    Alipokuwa Mwenyekiti wa FAT (sasa tuna Rais na TFF), Alhaji Muhiddin Ahmed Ndolanga alileta kocha Mjerumani mwaka 1998, Burkhad Pape.
    Lakini akaona kabisa kuna sehemu kocha huyo anakwama pamoja na weledi wake wa hali ya juu na uzoefu wake, hivyo akaamua kumfanya Mshauri wa Ufundi chini ya makocha Syllersaid Mziray (sasa marehemu) na Charles Boniface Mkwasa na timu ikatwaa Kombe la CECAFA Castle mwaka 2001 mjini Mwanza, wakiifunga Kenya 3-0 katika fainali mjini Mwanza, baada ya kuitoa DRC katika Nusu Fainali Arusha kwa penalti baada ya sare ya 2-2.
    Lakini sioni kama makocha Wasaidizi wa sasa, Salum Mayanga na Patrick Mwangata ni ambao wanaweza kuhimili uzito wa majukumu wa kuiongoza timu bila mtu juu yao.
    Maana yake, TFF lazima ihakikishe inapata kocha mwingine Mzungu, kama itaafiki kumuondoa Nooij. Na huyo kocha atakayekuja wiki mbili kabla ya kuanza mechi za kufuzu AFCON atafanya nini ndani ya muda huo mfupi? Huu ni mtihani mzito kwa TFF. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NOOIJ AMEIPA MTIHANI MZITO TFF, NI JUU YAO KUSUKA, AU KUNYOA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top