• HABARI MPYA

  Jumatano, Mei 27, 2015

  GEORGE WEAH NA MALINZI WAPANGA MKAKATI WA MAANA USWISI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MWANASOKA bora wa zamani wa Dunia, George Tawlon Manneh Oppong Ousman Weah, ameahidi kuziuganisha Tanzania na Liberia zishirikiane katika masuala ya maendeleo kisoka.
  Mshambuliaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Liberia amekutana na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi mjini Zurich, Usiwisi katika Mkutano wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) jana na kujadiliana mambo kadhaa.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY kwa simu leo kutoka Zurich, Malinzi amesema kwamba kubwa walilozungumzia ni ushirikiano katika nyanja za kimaendeleo baina ya nchi hizo.
  “Weah kama Nahodha wa zamani wa Liberia na mwanasiasa mkubwa nchini mwake, ameahidi kulifanikisha hilo,”amesema Malinzi.
  George Weah kulia akiwa Malinzi mjini Zurich, Uswisi jana 

  Rais huyo wa TFF amesema atakuwa na mikutano nje ya Mkutano wa CAF na wadau mbalimbali wakubwa wa soka Afrika kuomba msaada kwa ajili ya Tanzania.
  “Tunakutana viongozi wote wa FA za soka barani, lakini pia kuna wadau wengine wakubwa kama Weah. Nataka kutumia fursa hii kuwashawishi waweze kutusaidia kwa namna moja au nyingine,”amesema.  
  “Ni mambo mengi sana. Kwa mfano Liberia tu kukubali kutupa mechi za vijana za kirafiki na hata wakubwa, ili kubadilishana uzoefu, hilo nalo ni kubwa. Ila ni mambo mengi sana ninayohangaikia huku,”amesema Malinzi.
  George Weah enzi zake akiwa na tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia mwaka 1995
  Weah aliyezaliwa Oktoba 1 mwaka 1966 ni mmoja kati ya wanasoka bora zaidi kuwhai kutokea Afrika. Ndiye Mwafrika pekee kuwahi kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia mwaka 1995. Amekuwa Mwanasoka Bora wa Afrika katika miaka ya 1989, 1994 na 1995. Mwaka 2004 alitajwa kwenye orodha ya wanasoka 100 babu kubwa duniani walio hai.
  Weah alicheza kwa miaka 14 Ulaya katika nchi za Ufaransa, Italia na England na ni kocha wa sasa wa Arsenal, Arsene Wenger aliyempeleka Ulaya akimsajili Monaco mwaka 1988 kabla ya kuhamia Paris Saint Germain mwaka 1992 ambako alishinda mataji ya Ligue 1 mwaka 1994 na kuibuka mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa msimu wa 1994–1995. 
  Akasajiliwa na A.C. Milan mwaka 1995 ambako alikuwa na misimu minne mizuri mno, akifunga mabao muhimu la kukumbukwa zaidi ni dhidi ya Verona, na akashinda mataji mawili ya Serie A. Akahamia Ligi Kuu ya England kumalizia soka yake ambako alicheza Chelsea na Manchester City.
  Baada ya kustaafu soka, Weah amehamia kwenye siasa nyumbani kwao Liberia na mwaka 2005 aligombea Urais akashindwa na Ellen Johnson Sirleaf katika kura za marudio. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: GEORGE WEAH NA MALINZI WAPANGA MKAKATI WA MAANA USWISI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top