• HABARI MPYA

  Jumapili, Mei 24, 2015

  BENDI ZA ‘COPY’ KABURI LA BENDI ZINAZOISHI KWA TUNGO ZAO

  MIEZI michache iliyopita nilibahatika kualikwa kwenye kipindi cha taarab cha “Kwa Raha Zetu” cha Clouds FM kinachoendeshwa na mmoja wa watangazaji mahiri – Gea Habib.
  Kipindi hicho kinaruka kila siku za Jumapili saa 12 hadi 3 usiku, nikapata wasaa wa kubadilishana mawili matatu na Gea lakini kubwa tukazungumzia namna mahudhurio ya mashabiki wa muziki wa taarab yanavyoshuka ukumbini. Nilimpa sababu mbili. 
  Mosi:Upendo na ushirikiano kwa wasanii na bendi za taarabu kwa ujumla wake ni sifuri.
  Pili: kuwepo kwa utitiri wa bendi za kupiga muziki wa kunakili (copy) kwa kiingilio cha kinywaji chako. Sababu hii ya pili ndio mada yangu ya leo.
  Nilimwambia Gea haiwezekani Jahazi Modern Taarab ingurume pale Travertine Hotel Magomeni Mapipa kwa kiingilio cha shilingi elfu 7 halafu bendi ya copy iko Magomeni Mwembechai kwa kiingilio cha kinywaji chako ikipiga nyimbo zote kali za Jahazi, Mashauzi, Khadija Kopa na East African Melody. Hapo ni lazima Jahazi lidode.
  Huu ni utaratibu wa kienyeji ambao sasa umegeuzwa kuwa kitu rasmi, bendi zinaanzishwa huku hazina uwezo wa kutengeneza nyimbo zao wala uwezo wa kwenda studio badala yake zinaishi kwa kupiga nyimbo za bendi nyingine.
  Zamani sana tulizoea bendi za copy zikipiga kwenye mahoteli ya kitalii tena ziki-copy muziki wa nje lakini sasa imekuwa kinyume chake. Bendi nyingi za aina hiyo zimevamia uswahilini na kukomaa na nyimbo za bendi za hapa hapa nchini.
  Afadhali basi zingekuwa zinapiga ‘copy’ ya nyimbo za bendi zilizokufa, lakini kupiga nyimbo za bendi hai ni dhuluma ya wazi.
  Afadhali pia bendi hizo copy zingekuwa zinafanya kazi zao kwenye mji ambayo haina bendi, lakini kufanya kazi hizo jijini Dar es Salaam maskani ya bendi nyingi zinazohusika na kazi hizo zinaoibiwa ni uuaji wa kisanii.
  Hali hii ipo haipo kwenye bendi za taarab tu, ipo hata kwenye dansi. Bendi kama Malaika inaweza kuwa inapiga sehemu kwa kiingilio cha shilingi elfu 8 halafu hatua ishirini kutoka hapo unaiskia nyimbo “Nakuhitaji” inapigwa bureeee!
  Nimemskiliza malkia wa mipasho Khadija Kopa akiongea kitu hicho hicho cha kuzilalamikia bendi za copy katika mazungumzo yake na kipindi cha taarab cha TBC, nikafarijika kuona angalau sasa wasanii wanaonyonywa wameanza kuliona hilo.
  Hii kitu iko wazi kabisa wala haihitaji hata elimu ya shule msingi kubaini kuwa huu ni wizi – kutumia kazi ya mwezako bila ridhaa yake ili ujipatie pesa ni wizi, ni ufisadi, ni ushenzi.
  Ni lazima bendi ziungane katika hili na kukemea kwa nguvu uharamia huu uliofumbiwa macho kwa muda mrefu.
  Bendi zinatumia nguvu nyingi kuandaa nyimbo, kuhangaikia promosheni kwenye vyombo vya habari, gharama za kurekodi nyimbo studio, kisha mpuuzi mmoja anakaa kusuburi na kuangalia wimbo gani uko juu halafu bila woga wala haya anautumia kama mali yake.
  Msikubali bendi hizi za copy ziwe kaburi la soko lenu, fungueni macho, vyombo husika vipo na sheria zipo upande wenu, AMKENI.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BENDI ZA ‘COPY’ KABURI LA BENDI ZINAZOISHI KWA TUNGO ZAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top