• HABARI MPYA

  Jumanne, Mei 26, 2015

  YANGA SC YASAJILI KIPA WA MABORESHO NA BEKI LA KMKM

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imeendelea na usajili wa wachezaji wapya kuelekea msimu ujao na leo vifaa viwili vimemwaga wino makao makuu ya klabu, Jangwani.
  Beki wa kushoto Mwinyi Hajji Mngwali amesaini miaka miwili na kipa Benedicto Tinocco kutoka Kagera Sugar amesaini miaka mitatu.
  Tinocco ni kipa aliyeibuliwa mkoani Mara katika mpango wa maboresho ya timu ya taifa mwaka jana baadaye akasajiliwa Kagera Sugar ya Bukoba, wakati Mngwali ni mchezaji wa KMKM ya Zanzibar.   
  Tinocco yupo timu ya pili ya taifa, Taifa Stars Maboresho wakati Mngwali alikuwepo kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichocheza Kombe la COSAFA wiki mbili zilizopita.
  Beki mpya wa Yanga Mwinyi Hajji Mngwali akisaini mkataba wa kuitumikia klabu leo makao makuu ya klabu hiyo, Jangwani, Dar es Salaam. Wanaoshuhudia kutoka kulia ni Ofisa Masoko, Omary Kaaya, Meneja wa timu, Hafidh Saleh na Katibu Mkuu Dk Jonas Tiboroha.

  Kipa mpya wa Yanga, Benedicto Tinocco akiweka alama ya dole gumba katika mkataba wake wakati akisaini mkataba wa kuitumikia klabu hiyo leo Jangwani

  Mngwali alicheza mechi moja tu ya mwisho kwenye Kombe la COSAFA mjini Rusternburg, Afrika Kusini Taifa Stars ikilala 1-0 mbele ya Lesotho.
  Mechi zote mbili za mwanzo, ambazo Stars ilifungwa 1-0 na Swaziland na 2-0 na Madagascar, beki ya kushoto alicheza Oscar Joshua wa Yanga pia.
  Mwinyi sasa anakwenda kugombea kucheza beki ya kushoto ya Yanga pamoja na mabeki wengine wawili, Oscar Joshua na Edward Charles ambao wote wapo Taifa Stars.
  Tinocco pamoja na kusajiliwa Kagera Sugar msimu huu lakini hakuwa na nafasi kwenye kikosi cha kwanza, ingawa ameonyesha ni kipa mzuri na mwenye umbo zuri, ambaye kama atajibidiisha atakuwa bora baadaye.
  Tinocco anakwenda kugombea namba na makipa wazoefu wa Yanga SC, Ally Mustafa ‘Barthez’na Deogratius Munishi ‘Dida’, ambaye kwa sasa ni kipa chaguo la kwanza la Taifa Stars.     
  Wawili hao wanafanya idadi ya wachezaji wapya waliosajiliwa Yanga SC kufika watatu ndani ya suku tatu, baada ya juzi ilimsainisha winga wa Mbeya City, Deus Kaseke kwa miaka miwili.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC YASAJILI KIPA WA MABORESHO NA BEKI LA KMKM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top