• HABARI MPYA

    Wednesday, May 13, 2015

    JEMADARI ABWAGA MANYANGA AZAM FC, ALAMBA AJIRA TFF

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Jemadari Said Kazumari ameachana na Azam FC na kuchukua ajira Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
    Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba Jemadari ameajiriwa kama Ofisa Maendeleo wa shirikisho, wadhifa ambao ataanza kuutumikia Juni 1.
    Mchezaji huyo aliyewika Kariakoo United ya Lindi mwaka 1999 hadi 2002, ametua TFF baada ya kumaliza Mkataba wake katika klabu ya Azam FC kama Meneja.
    Jemadari anaondoka Azam FC, akiwa anajivunia mafanikio ya kuiwezesha timu kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita.
    Marafiki siku nyingi; Jemadari akiwa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi (kulia) mwaka jana katika usiku wa utoaji wa tuzo za Ligi Kuu

    Msimu huu, Jemadari ameiacha Azam FC katika nafasi ya pili, nyuma ya mabingwa wapya Yanga SC. 
    Lakini tayari uongozi wa Azam FC umefikia uamuzi wa kuondoa benchi lote la Ufundi la sasa na kulihamishia katika timu za vijana za klabu hiyo. Kocha Muingereza Stewart John Hall anakuja timu A na timu kamili ya makocha wa kufanya nao kazi.
    Hall ambaye awali aliifundisha Azam FC kwa awamu mbili, anakuja na Kocha Msaidizi, kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili na kocha wa makipa kuanza kuiandaa timu kwa ajili ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.
    Michuano hiyo maarufu kama Kombe la Kagame inatarajiwa kuanza Julai 11 mjini Dar es Salaam na baada ya Azam FC kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu msimu huu, imevunja benchi la Ufundi.
    Aliyekuwa kaimu kocha Mkuu, Mganda George ‘Best’ Nsimbe na timu yake nzima, Dennis Kitambi, Iddi Abubakar kocha wa makipa na wenginw wanakwenda Azam Akademi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JEMADARI ABWAGA MANYANGA AZAM FC, ALAMBA AJIRA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top