• HABARI MPYA

    Thursday, May 14, 2015

    STARS YAWASILI RUSTENBURG TAYARI KWA COSAFA

    Na Mahmoud Zubeiry, RUSTENBURG
    TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imewasili mchana wa leo mjini Rustenburg, Afrika Kusini tayari kwa michuano ya Kombe la COSAFA inayoanza Jumapili.
    Stars iliwasili Johannesburg, Afrika Kusini usiku wa jana na ikalazimika kulala huko kabla ya leo asubuhi kuunganisha safari kwa basi kuja Rosenborg ambako imefikia hoteli ya Hunters, nje kidogon ya mji.
    Kiungo mshambuliaji, Mrisho Khalfan Ngassa aliyekuwa mjini Bethlehem kusaini Mkataba na timu yake mpya, Free State Stars ya Ligi Kuu Afrika Kusini ameungana wenzake hapa.
    Mshambuliaji wa Taifa Stars, Simon Msuva akiwasili hoteli ya Hunters mjini Rustenburg leo 

    Ikumbukwe, Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ameondolewa kikosini baada ya kugundulika bado majeruhi.  Majeruhi wengine walioondolewa Taifa Stars ni Aishi Manula, Isihaka Hassan, Haroun Chanongo na Kelvin Friday, wakati kiungo Amri Kiemba amepewa ruhusa kutokana na kuwa na matatizo ya kifamilia.
    Michuano ya COSAFA inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Mei 17 mpaka Mei 30, 2015 katika viwanja vya Olympia Park na Moruleng, ikishirikisha nchi za Kusini mwa Afrika huku Tanzania na Ghana zikiwa ni nchi waalikwa.
    Wachezaji waliowasili na Stars hapa ni makipa: Deogratius Munish ‘Dida’ (Yanga) na Mwadini Ali (Azam), mabeki ni Shomary Kapombe, Aggrey Morris, Erasto Nyoni (Azam), Oscar Joshua, Kelvin Yondani (Yanga), Abdi Banda, Salim Mbonde (Mtibwa Sugar) na Mwinyi Hajji Mngwali (KMKM).
    Wengine ni viungo; Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Domayo (Azam), Said Juma, Salum Telela, Hassan Dilunga (Yanga), Said Ndemla (Simba) na Mwinyi Kazimoto (Al Markhiya, Qatar).
    Washambuliaji ni Ibrahim Hajib (Simba), Mrisho Ngassa (Free State Stars), Simon Msuva (Yanga), John Bocco (Azam FC) na Juma Luizio (Zeco United).
    Kutoka kulia Erasto Nyoni, Msuva, Shomary Kapombe na Hassan Dilunga

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS YAWASILI RUSTENBURG TAYARI KWA COSAFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top