• HABARI MPYA

    Tuesday, July 15, 2014

    KOCHA BUSH WA KMKM AFURAHIA KUPANGWA KUNDI MOJA NA YANGA YA MAXIMO KAGAME

    Na Salum Vuai, ZANZIBAR
    KOCHA mkuu wa klabu ya KMKM Ali Bushiri ‘Bush’, amesema amefarijika kupangwa pamoja na Yanga SC katika mashindano ya Kombe la Kagame yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 8, mwaka huu mjini Kigali, Rwanda.
    Bushiri amesema kuwa, furaha yake inatokana zaidi na kwamba Yanga inafundishwa na bosi wake wa zamani katika timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars, Mbrazili Marcio Maximo.
    Kocha huyo wa KMKM alikuwa msaidizi wa Maximo kabla kuondolewa kwenye timu hiyo ya taifa baada ya Mbrazili huyo kumaliza mkataba wake kuinoa Taifa Stars.
    Kocha wa KMKM, Ali Bushiri amefurahia kupangwa na Yanga SC Kombe la Kagame 

    Alisema, kwa timu yake kuwa katika kundi moja na Yanga, ni changamoto nzuri kwake, kwani atapata fursa ya kudhihirisha ukomavu wake mbele ya mwalimu Maximo, ambaye walipokuwa pamoja Taifa Stars, Bushiri alijifunza mengi kutoka kwake na kuchota utaalamu unaomsaidia hadi sasa.
    “Nimefurahi sana kuwa katika kundi moja na Yanga ambayo inafundishwa na bosi wangu wa zamani. Ninamheshimu Maximo, ni rafiki na mwalimu wangu ambaye tangu ameondoka nchini bado tunawasiliana kwa mengi,” alisema Bushiri.
    “Lakini, pamoja na hayo hii ni fursa adhimu ya kupimana ubavu na kudhihirisha mikoba aliyoniachia ninaitumia vyema, vitakuwa vita vikali,” aliongeza Bushiri, mlinda
    mlango wa zamani wa Small Simba, Malindi SC na timu za taifa Zanzibar na Tanzania.  
    “Maximo ataendelea kuwa bosi wangu katika kazi, na nitaendelea kumuheshimu kwa kuwa alinitoa sehemu ya chini na kunipandisha juu kitaaluma katika ufundishaji, lakini kwa kukutana timu zetu kwenye mashindano haya nadhani ni mtihani mzuri kwangu ili aone jinsi nilivyoshika na kutumia taaluma aliyonipa  hadi kuweza kutwaa ubingwa wa ligi kuu mara mbili,” alifafanua Bushiri.
    Bushiri aliyeibuka kocha bora wa ligi kuu ya Zanzibar msimu uliopita na kuzawadiwa shilingi milioni moja na kinywaji cha Grand Malt, alisisitiza kwamba mbali na Maximo, pia anaiheshimu Yanga na kueleza kuwa mchezo kati yao utakuwa mzuri na wa kiushindani.
    Bushiri kulia akiwa ma Maximo karikati wakati wakiranya kazi pamoja Taifa Stars. Kushoto ni aliyekuwa Meneja, Leopold Mukebezi 'Taso'

    Akizungumzia timu zilizoko kundi ‘A’ pamoja na timu yake kwa jumla, Bushiri alikiri kuwa kundi hilo ni gumu, lakini hiyo haina maana watashindwa kupambana na kupata mafanikio.
    Alieleza kuwa timu zote hizo si ngeni kwani wanazifahamu na uchezaji wao, na kwamba binafsi amefurahi kuwemo kwenye kundi hilo kwani litawapa changamoto na kuleta ushindani mzuri.
    Aidha alijigamba kuwa anawaamini vijana wake ambao alisema wameonesha kuimarika vizuri tangu walipoanza mazoezi wiki tano sasa kujiandaa kwa ligi kuu na mashindano ya kimataifa.
    Katika mashindano hayo yanayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), mabingwa hao wa ligi kuu Zanzibar wako katika kundi ‘A’ pamoja na timu za Yanga SC, Rayon Sports (Rwanda), Coffee (Ethiopia) na Altbara (Sudan Kusini).
    Kundi ‘A’ linaundwa na timu za APR ya Rwanda, KCC (Uganda), Flambeau De’ast (Burundi), Gor Mahia (Kenya) na Telecom ya Djibouti.
    Timu za kundi ‘C’ ni Vital’O (Burundi), El Mirreikh (Sudan), Polisi (Rwanda) na Bandari ya Somalia.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KOCHA BUSH WA KMKM AFURAHIA KUPANGWA KUNDI MOJA NA YANGA YA MAXIMO KAGAME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top