• HABARI MPYA

  Sunday, February 04, 2018

  SIMBA SC YAIMIMINIA RUVU SHOOTING 3-0 BOCCO APIGA MBILI…OKWI AUMIA KIPINDI CHA KWANZA NA KUTOLEWA

  Na Mahmoud Zubeiry, DARES SALAAM
  SIMBA SC imeendeleza kasi yake nzuri kuelekea kwenye taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ruvu Shooting jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Ushindi huo unaifanya Simba ifikishe pointi 38 baada ya kucheza mechi 16 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi tano zaidi ya Azam FC wanaoshika nafasi ya pili huku pia wakiwazidi pointi saba mabingwa watetezi, Yanga SC walio nafasi ya tatu.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Hans Mabena wa Tanga aliyesaidiwa na Arnold Bugando wa Singida na Slyvester Mwanga wa Kilimanjaro, hadi mapumziko Simba ilikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Wafungaji wa mabao ya Simba leo, Muzalim Yassin (kulia) na John Bocco (katikati) wakipongezana kwa pamoja na mpishi wa bao la pili, Shiza Kichuya
  Emmanuel Okwi (kushoto) akimiliki mpira kwa kichwa dhidi ya beki wa Ruvu Shooting
  John Bocco akiruka juu kupiga kichwa dhidi ya wachezaji wa Ruvu Shooting
  Shomary Kapombe akiwania mpira wa juu na mchezaji wa Ruvu Shooting 
  Beki wa Simba, Asante Kwasi akimdhibiti mchezaji wa Ruvu Shooting leo

  Bao hilo lilifungwa na Nahodha John Raphael Bocco dakika ya 22 akitumia vizuri urefu wake kutumbukiza mpira nyavuni kwa kichwa baada ya kona ya winga Shiza Ramadhani Kichuya kutoka upande wa kulia. 
  Simba SC iliongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa Ruvu Shooting kusaka mabao zaidi, lakini ikaishia kukosa mabao ya wazi na almanusra Bocco afunge bao lingine dakika ya 44 kama si mpira aliopiga kwa kichwa tena kumalizia krosi ya beki wa kulia, Shomary Kapombe kwenda nje sentimita chache.
  Ruvu ikapata pigo dakika ya 45, baada ya beki wake, Mau Bofu kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu mbaya mshambuliaji Mganda, Emmanuel Arnold Okwi aliyeshindwa kuendelea na mchezo na nafasi yake kuchukuliwa na Mrundi, Laudit Mavugo.
  Kipindi cha pili, Simba ya kocha Mfaransa Pierre Lechantre anayesaidiwa na Mrundi, Masoud Juma ilikianza na mabadiliko, ikipumzisha kiungo chipukizi Said Hamisi Ndemla na kumuingiza mkongwe Mwinyi Kazimoto Mwitula na Ruvu Shooting ya kocha Mzanzibari Abdulmatik Haji anayesaidiwa na mzalendo mwenzake, Suleiman Kidungwe ilimuingiza Yussuph Nguya kuchukua nafasi ya Issa Kandulu.
  Mabadiliko hayo hayo yaliinufaisha Simba SC na kufanikiwa kupata mabao mawili zaidi, Bocco akifunga bao lake la tisa la msimu katika Ligi Kuu sasa anazidiwa matatu tu na, Okwi  anayeongoza kwa mabao yake 12. 
  Lakini ni kiungo Muzamil Yassin aliyefunga bao la pili dakika ya 66 akimalizia krosi nzuri ya winga Shiza Kichuya waliyesajiliwa pamoja Simba SC msimu uliopita kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro,
  Bocco aliye katika msimu wake wa kwanza Simba SC tangu asajiliwe kutoka Azam FC Julai mwaka jana akakamilisha shangwe za mabao za Simba leo kwa kufunga bao la tatu dakika ya 75 akitumia vizuri makosa ya kipa Abdallah Rashid kutoka bila mahesabu.
  Ruvu Shooting wakapata pigo lingine dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya kutimia dakika za kawaida za mchezo, kufuatia mchezaji wake, Adam Ibrahim kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Kichuya.
  Kikosi cha Ruvu Shooting kilikuwa; Abdallah Rashid, George Aman, Mau Bofu, Damas Makwaya, Rajab Zahir, Baraka Mtui, Abdulrhaman Mussa, Adam Ibrahim, Issa Kanduru/Yuzssuph Nguya dk46, Shaaban Msala na Fully Zulu Maganga/Jamal Soud dk61.
  Simba SC; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Asante Kwasi, Erasto Nyoni, Yusuph Mlipili, Jonas Mkude, Emmanuel Okwi/Laudit Mavugo dk45, Said Ndemla/Mwinyi Kazimoto dk46, John Bocco/Nicholas Gyan dk78, Muzamil Yassin na Shiza Kichuya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAIMIMINIA RUVU SHOOTING 3-0 BOCCO APIGA MBILI…OKWI AUMIA KIPINDI CHA KWANZA NA KUTOLEWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top