• HABARI MPYA

  Wednesday, January 18, 2017

  SIMBA NA MTIBWA SUGAR NI KIVUMBI JAMHURI LEO

  Na Mwandishi Wetu, MOROGORO
  VINARA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba SC leo watajaribu kusogea mbali na wapinzani wao wakuu katika mbio za ubingwa, Yanga SC.
  Simba SC watakuwa wageni wa Mtibwa Sugar katika mfululizo wa Ligi Kuu Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
  Na baada ya Yanga kushinda 1-0 dhidi ya wenyeji Maji Maji Uwanja wa Maji Maji mjini Songea mkoani Ruvuma jana, iliikaribia Simba kwa tofauti ya moja kutoka nne.
  Sasa Simba leo watakuwa na jukumu la kupigania ushindi ili kurudisha gepu la pointi nne na kendelea kuongoza vizuri mbio za ubingwa wa Ligi Kuu wakiwaacha mbali mabingwa hao watetezi.
  Lakini hilo halitarajiwi kuwa jepesi kutokana na hali halisi ya kikosi cha Mtibwa Sugar kwa sasa na dhamira yao ya kutotaka kupoteza mechi – pamoja na historia ya mechi za timu hizo, huwa kali na zisizotabirika.
  Na tayari Mtibwa Sugar wamekwishasema kupitia kwa Msemaji wao maarufu, Thobias Kifaru kwamba; “Simba hawatoki Jamhuri”.
  Lakini upande wa Simba napo, chini ya Kocha Mkuu, Mcameroon Joseph Marius Omog dhamira yao ni kucheza kila mechi kama fainali kuhakikisha wanashinda.
  Omog anaamini Simba inakamiwa kila mechi na ili kushinda ni lazima kucheza kama fainali kwa kupigana kwa nguvu zote mwanzo hadi mwisho wa mchezo.
  Na bila shaka hiyo ndiyo siri ya mafanikio ya Simba hata imeweza kuongoza Ligi Kuu kwa muda mrefu msimu huu.
  Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo unatarajiwa kufanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kati ya wenyeji, Azam FC dhidi ya Mbeya City.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA NA MTIBWA SUGAR NI KIVUMBI JAMHURI LEO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top