• HABARI MPYA

  Friday, January 13, 2017

  MALINZI AMPONGEZA MKURUGENZI MPYA WA MICHEZO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amempongeza Yusuph Singo Omari kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Tanzania.
  Mapema wiki hii, Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo ilimteua Yusuph Singo Omari kuchukua nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Leonard Thadeo aliyehamishiwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
  Kabla ya uteuzi huo uliofanywa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 kifungu namba 6, kifungu (1) (b) kikisomwa pamoja na kifungu namba 8 cha sheria hiyo, Bw. Yusuph Singo Omari alikuwa Mkufunzi Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Ardhi katika masuala ya Michezo.
  Katika pongezi zake, Rais Malinzi amepokea wito wa Waziri Nape Nnauye kumpa ushirikiano wa kutosha kwa Yusuph Singo Omari atakapokuwa anatekeleza majukumu yake.
  “Sisi wa TFF tunakupongeza kwa nafasi hiyo, tunachukua nafasi hii kukuahidi kukupa ushirikiano wa kutosha katika majukumu yako mapya. Hii ni kuitikia wito wa Wizara ambayo imeomba wanafamilia yote ya michezo kukupa ushirikiano,” alisema Malinzi.
  Rais Malinzi alisema kwamba program za TFF kwa sasa kwa timu zake zote za taifa, hazina budi kuungwa mkono na Serikali ili kufanikisha na kiungo mkubwa katika eneo hilo ni Yusuph Singo Omari ambaye ndiye mkuu wa Idara ya Maendeleo ya michezo – mpira wa miguu ukiwa ni miongoni mwa michezo hiyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MALINZI AMPONGEZA MKURUGENZI MPYA WA MICHEZO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top