• HABARI MPYA

  Friday, January 13, 2017

  AZAM BINGWA MAPINDUZI 2017, SIMBA VITANDANI MAPEMAAA!

  Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR
  AZAM imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi 2017, baada ya kuwachapa Simba 1-0 usiku huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Shukrani kwake kiungo Himid Mao Mkami aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 12 kwa shuti kali la umbali wa mita 25 baada ya kupokea pasi ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
  Baada ya pasi ya Sure Boy, Himid alisogea hatua mbili mbele akatisha kama anapiga, akasogea tena hatua moja na kupiga shuti kali lililompita kipa Mghana wa Simba, Daniel Agyei.
  Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein (kushoto) akimkabidhi Nahodha wa Azam, John Bocco Kombe la ubingwa wa Mapinduzi 
   Wachezaji wa Azam wakifurahia na Kombe lao la ubingwa wa Mapinduzi 
  Mfungaji wa bao pekee la ushindi la Azam, Himid Mao (katikati) akifurahia na mashabiki

  Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa, Mafume Ali Nassor nafasi nzuri zaidi ambyo Simba waliipata ni dakika ya 27 baada ya beki Abdi Banda kupiga shuti la mpira wa adhabu umbali wa mita 22, lakini kipa Aishi Manula akajituma kulifuata pembezoni mwa lango kushoto na kutoa nje.
  Kipindi cha kwanza mabeki wa Azam walikuwa wana kazi rahisi ya kumdhibiti mshambuliaji pekee wa Simba, Juma Luizo, lakini kipindi cha pili walifanya kazi ya ziada baada ya kuongezeka Mrundi Laaudit Mavugo.
  Hilo linakuwa taji la tatu la Kombe la Mapinduzi kwa Azam FC baada ya awali kutwaa katika miaka ya 2012 na 2013, hivyo kufikia rekodi ya Simba waliokuwa wanaongoza kwa kutwaa mara nyingi katika miaka ya 2008, 2011 na 2015. 
  Sifa zaidi kwa Kocha aliyeiongoza Azam katika mashindano haya, Iddi Nassor ‘Cheche’ baada ya kufukuzwa kwa Waspaniola chini ya Zeben Hernandez Rodriguez ambaye ameweka rekodi ya kutofungwa hata bao moja.
  Azam pia imeendeleza rekodi yake ya kuchukua Kombe hilo mara zote ilizoingia, wakati kwa Simba hii ni mara ya tatu wanaingia fainali bila kuchukua Kombe kama mwaka 2012 na 2014.
  Ushindi huo Azam walizawadiwa Sh. Milioni 10 na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, wakati Simba walipata Sh. Milioni 5.
  Kipa Bora wa Mashindano ni Aishi Manula, Beki Bora ni Mzimbabwe Method Mwanjali wa Simba na Mfungaji Bora ni Simon Msuva wa Yanga.
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa: Aishi Manula, Shomary Kapombe, Gadiel Michael, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Stephan Kingue,Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Himid Mao/Enock Atta Agyei dk82, John Bocco, Yahya Mohammed/Mudathir Yahya dk68 na Joseph Mahundi/Frank Domayo dk57. 
  Simba SC: Daniel Agyei, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, James Kotei, Method Mwanjali, Shiza Kichuya/Jamal Mnyate dk76, Juma Luizio, Muzamil Yassin/Pastory Athanas dk71 na Mwinyi Kazimoto/Laudit Mavugo dk42.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM BINGWA MAPINDUZI 2017, SIMBA VITANDANI MAPEMAAA! Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top