• HABARI MPYA

    Sunday, March 07, 2021

    YANGA SC YAPOKONYWA TONGE MDOMONI ARUSHA, YALAZIMISHWA SARE YA 1-1 NA POLISI TANZANIA

    Na Mwandishi Wetu, ARUSHA
    VINARA, Yanga SC leo wamelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, Polisi Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.
    Kwa sare hiyo, Yanga SC inayofundishwa na kocha Mrundi, Cedric Kaze inafikisha pointi 50 baada ya kucheza mechi 23 ikiendelea kuongoza ligi kwa pointi tano zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC. 
    Yanga SC walitangulia kwa bao la mshambuliaji Mrundi, Fiston Abdul Razak dakika ya 42 akimalizia kwa kisigino krosi ya winga Mkongo, Tuisila Kisinda kutoka upande wa kulia.

    Lakini kiungo wa zamani wa Yanga, Pius Buswita aliyetokea benchi kipindi cha pili akaisawazishia Polisi Tanzania dakika ya 90 akimalizia kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Deusdedit Cossmas.
    Polisi ilimaliza pungufu baada ya beki wake, mkongwe Kelvin Yondani kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 87 kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
    Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Gwambina FC imeibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, mabao ya Paul Nonga dakika ya 24 na Hamad Nassor dakika ya 71 Uwanja wa CCM Gairo mkoani Morogoro. 
    Nayo Coastal Union imelazimishwa sare ya bila kufungana na KMC katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
    Kikosi cha Polisi Tanzania kilikuwa; Mohamed Yussuf, Datius Peter, Juma Ramadhani, Iddy Moby, Kelvin Yondan, Pato Ngonyani, Daruwesh Saliboko, Nassor Maulid, Tariq Seif Kiakala, Kassim Shaaban/Pius Buswita dk61 na Marcel Kaheza/Gerald Mathias dk54.
    Yanga SC; Metacha Mnata, Kibwana Shomari/Waziri Junior dk90+2, Yassin Mustapha, Said Juma ‘Makapu’, Bakari Mwamnyeto, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Feisal Salum, Fiston Abdul Razak, Haruna Niyonzima na Ditram Nchimbi/Deus Kaseke dk61.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC YAPOKONYWA TONGE MDOMONI ARUSHA, YALAZIMISHWA SARE YA 1-1 NA POLISI TANZANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top