• HABARI MPYA

  Monday, March 01, 2021

  MIQUISSONE AFUNGA BAO MOJA NA KUSETI MOJA SIMBA SC YAWACHAPA JKT TANZANIA 3-0 LIGI KUU DAR

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi, Simba SC wameendelea kuwapa raha mashabiki na wapenzi wao baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi ya Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo, Simba SC inayofundishwa na kocha Mfaransa, Didier Gomes Da Rosa anayesaidiwa na Mzalendo, Suleiman Matola inafikisha pointi 45 baada ya kucheza mechi 19, ingawa inabaki nafasi ya pili, ikizidiwa pointi nne na vinara, Yanga SC ambao hata hivyo wamecheza mechi mbili zaidi.
  Kiungo wa kimataifa wa Msumbiji, Luis Jose Miquissone ameendelea kuwa nyota mwenye mchango mkubwa kikosini baada ya kufunga bao moja na kuseti moja kipindi cha kwanza.
  Miquissone aliyezaliwa miaka 25 iliyopita, alianza kumsetia mshambuliaji Mkongo, Chris Mutshimba Kope Mugalu kufunga bao la kwanza dakika ya nane kabla yay eye mwenyewe mchezaji huyo wa zamani wa UD Songo ya kwao, Msumbiji na Mamelodi Sundowns, Chippa United na Royal Eagles za Afrika Kusini kufunga la pili dakika ya 37 akimalizia pasi ya beki mzawa, Erasto Edward Nyoni.
  Simba SC ikapata pigo dakika ya 70 baada ya kipa namba moja Tanzania, Aishi Salum Manula kushindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia kufuatia kugongana na mshambuliaji wa JKT, Daniel Lyanga na nafasi yake kuchukuliwa Beno David Kakolanya aliyekwenda kumalizia vizuri mchezo.
  Nahodha na mshambuliaji mzawa, John Raphael Bocco akaifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 90 akimalizia pasi ya mtokea benchi mwenzake leo, kiungo Mzambia Rally Bwalya.
  Baada ya mchezo huo, Simba SC watasafiri kwenda Sudan kwa ajili ya mchezo wao wa tatu wa Kundi A Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, El Merreikh Jumamosi Uwanja wa Al-Hilal Jijini Omdurman.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula/Beno Kakolanya dk70, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Kennedy Juma, Clatous Chama, Thadeo Lwanga, Chriss Mugalu/John Bocco dk66, Muzamil Yassin na Luis Miquissone/Rally Bwalya dk68.
  JKT Tanzania; Patrick Muntary, Saad Abubakar, Paul Ngalema, Edson Katanga, Hamad Waziri, Nurdin Mohamed/Kiggy Makassy dk58, Kelvin Nashon, Hafidh Mussa/Rashid Mandawa dk58, Daniel Lyanga, Edward Songo na Shaaban Mgandila/Mussa Said dk88.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MIQUISSONE AFUNGA BAO MOJA NA KUSETI MOJA SIMBA SC YAWACHAPA JKT TANZANIA 3-0 LIGI KUU DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top