• HABARI MPYA

  Sunday, March 07, 2021

  YANGA SC YAVUNJA BENCHI ZIMA LA UFUNDI BAADA YA KULAZIMISHWA SARE NA POLISI TANZANIA LEO ARUSHA

  Na Mwandishi Wetu, ARUSHA
  KLABU ya Yanga SC leo imetangaza kumfuta kazi kocha wake, Mrundi Cedric Kaze pamoja na wasaidizi wake wote kwa sababu ya matokeo mabaya.
  Pamoja na Kaze, wengine wanaoondoka ni Kocha Msaidizi, mzawa Nizar Khalfan, Kocha wa Makipa Vladimir Niyonkuru, Kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili, Mghana Edem Mortolsi na Afisa Usalama wa kambi, Mussa Mahundi.
  Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Yanga kulazimishwa sare ya 1-1 na wenyeji, Polisi Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jana Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.


  Kwa sare hiyo inayozidi kupunguza matumaini ya ubingwa Yanga SC ikifikisha pointi 50 baada ya kucheza mechi 23 na kuendelea kuongoza ligi kwa pointi tano zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC ambao hata hivyo wana mechi tatu mkononi. 
  Juzi Yanga SC walitangulia kwa bao la mshambuliaji Mrundi, Fiston Abdul Razak dakika ya 42 akimalizia kwa kisigino krosi ya winga Mkongo, Tuisila Kisinda kutoka upande wa kulia.
  Lakini kiungo wa zamani wa Yanga, Pius Buswita aliyetokea benchi kipindi cha pili akaisawazishia Polisi Tanzania dakika ya 90 akimalizia kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Deusdedit Cossmas.
  Polisi ilimaliza pungufu baada ya beki wake, mkongwe Kelvin Yondani kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 87 kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
  Na kazi anaondoka Yanga SC baada ya kuiongoza timu katika mechi 25 tangu awasili Oktoba, mwaka jana kuchukua nafasi ya Mserbia, Zlatko Krampotic akiwa ameshinda mechi 15, kati ya hizo mbili kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Azam na Simba baada ya sare katika Kombe la Mapinduzi.
  Kaze amefungwa mbili dhidi ya timu za Tanga tupu, African Sports 1-0 Jijini Dar es Salaam ya kirafiki na Coastal Union 2-1 Tanga ya Ligi Kuu, wakati nyingine nane ametoka droo nane. 

  MECHI ZA YANGA CHINI YA CEDRIC KAZE
  1. Yanga SC 1-0 Polisi Tanzania (Ligi Kuu Uhuru)
  2. Yanga SC 2-1 KMC (Ligi Kuu Kirumba)
  3. Yanga SC 1-0 Biashara United (Ligi Kuu Musoma)
  4. Yanga SC 0-0 Gwambina FC (Ligi Kuu Misungwi)
  5. Yanga SC 1-1 Simba FC (Ligi Kuu Mkapa)
  6. Yanga SC 3-1 African Lyon (Kirafiki Chamazi)
  7. Yanga SC 1-1 Namungo FC (Ligi Kuu Mkapa)
  8. Yanga SC 1-0 Azam FC (Ligi Kuu Chamazi)
  9. Yanga SC 1-0 JKT Tanzania (Ligi Kuu Mkapa)
  10. Yanga SC 2-1 Ruvu Shooting (Ligi Kuu Mkapa)
  11. Yanga SC 5-0 Mwadui FC (Ligi Kuu Kambarage)
  12. Yanga SC 3-0 Singida United (Kirafiki Malkia Liti, Singida)
  13. Yanga SC 3-1 Dodoma Jiji FC (Ligi Kuu, Sheikh Amri Abeid)
  14. Yanga SC 3-0 Ihefu SC (Ligi Kuu, Sokonie)
  15. Yanga SC 1-1 Tanzania Prisons (Ligi Kuu, Sumbawanga)
  16. Yanga SC 0-0 Jamhuri FC (Kombe la Mapinduzi, Zanzibar)
  17. Yanga SC 1-1 (Penalti 5-4) Azam FC (Nusu Fainali Kombe la Mapinduzi, Zanzibar)
  18. Yanga SC 0-0 (Penalti 4-3) Yanga SC (Fainali Kombe la Mapinduzi, Zanzibar)
  19. Yanga SC 0-1 African Sports (Kirafiki Chamazi)
  20. Yanga SC 1-1 Mbeya City (Ligi Kuu Sokoine)
  21. Yanga SC 3-3 Kagera Sugar (Ligi Kuu Mkapa)
  22. Yanga SC 1-0 Mtibwa Sugar (Ligi Kuu Mkapa)
  23. Yanga SC 1-0 Ken Gold (Kombe la TFF Uhuru)
  24. Yanga SC 1-2 Coastal Union (Ligi Kuu Mkwakwani)
  25. Yanga SC 1-1 Polisi Tanzania (Ligi Kuu Arusha)

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YAVUNJA BENCHI ZIMA LA UFUNDI BAADA YA KULAZIMISHWA SARE NA POLISI TANZANIA LEO ARUSHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top