• HABARI MPYA

  Ijumaa, Machi 19, 2021

  MAMA SAMIAH SULUHU HASSAN AAPISHWA KUWA RAIS WA SITA WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA


  Samia Suluhu Hassan aapishwa kuwa Rais wa Tanzania na Jaji Ibrahim Juma katika Ikulu ya Jijini Dar es Salaam.

  Mama Samia ameapishwa katika hafla ndogo iliyofanyika katika Ikulu ya Magogoni na kuhudhuriwa na marais wastaafu wa Tanzania na Zanzibar.

  Mara baada ya kuapishwa alipigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride maalumu kwa mara ya kwanza akiwa kama amiri jeshi mkuu wa majeshi ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.

  Mama Samia mwenye miaka 61, ndio mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huu nchini Tanzania na wa pili Afrika Mashariki.

  Slyvie Kiningi ndiye alikuwa rais wa pekee mwanamke aliyeshika nyadhifa ya urais Afrika Mashariki nchini Burundi.

  Mama Samia ameapishwa kushika wadhifa huo kufuatia kifo cha rais John Pombe Magufuli kilichotokea Jumatano, Machi 17, 2021.

  Rais Samia atashikilia wadhifa huo kwa kipindi kilichosalia cha muhula wa urais mpaka 2025, kwa mujibu wa katiba ya Tanzania.

  Maelezo ya video,

  Samia Suluhu Hassan aapishwa kuwa Rais wa Tanzania

  Hotuba ya kwanza ya Rais Samia Suluhu Hassan

  Katika hotuba yake ya kwanza baada ya kuapishwa kuwa rais wa awamu ya sita, Rais Samia Suluhu Hassan amesema hakuna kitakachoharibika.

  "Amenifundisha mengi na amenilea na kuniandaa vya kutosha, tumepoteza kiongozi shupavu. Alikua chachu ya mabadiliko"Rais Samia amesema.

  Rais pia alieleza pia kwa hisia namna ambavyo kuchukua kwake hatamu kumekuwa kugumu kwake.

  "Leo nimekula kiapo cha juu sana nikiwa na majonzi tele na kukiwa na simanzi kubwa mtaniwia radhi leo nitaongea kwa uchache sana mengine tutazungumza"

  samia

  Aidha Rais Samia amewataka watanzania kuzika tofauti zao.

  "Huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu na kuwa wamoja kama taifa, kufarijiana kuonyesha upendo, undugu wetu, kudumisha amani yetu, kuenzi utu wetu, uzalendo wetu na utanzania wetu."

  ''Si wakati wa kutazama yaliyopita lakini ni wakati wa kutazama yaliyo mbele. Huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu. Huu si wakati wakutazama mbele kwa mashaka bali kwa matumaini.si wakati wa kunyosheana vidole bali ni wakati wa kushikana mikono," Rais Samia ameeleza.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MAMA SAMIAH SULUHU HASSAN AAPISHWA KUWA RAIS WA SITA WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top