• HABARI MPYA

  Jumamosi, Novemba 09, 2019

  KMC YAMTUPIA VIRAGO MAYANJA MIEZI MITANO TU TANGU ARITHISHWE MIKOBA YA NDAYIRAGIJE

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya KMC ya Kinondoni mjini Dar es Salaam imemfuta kazi kocha wake, Mganda Jackson Mayanja miezi mitano tu aajiriwe.
  Mwenyekiti wa Bodi ya KMC Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta amesema kwamba wamefikia uamuzi huo kufuatia matokeo yasiyoridhisha tangu kuanza kwa msimu huu.
  “Tunamshukuru kocha Jackson Mayanja kwa mchango wake mkubwa alioutoa akiwa na timu. KMC inamtakia kila la heri katika majukumu yake,”amesema Meya Sitta katika taarifa yake jana usiku.

  Uamuzi huo ulifuatia KMC kufungwa 2-1 Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Matokeo hayo yanaifanya KMC ibaki na pointi zake nane baada ya kucheza mechi nane, ikiwa inashika nafasi ya 16 katika Ligi Kuu ya timu 16.
  Mayanja alijiunga na KMC Juni 26, mwaka huu akichukua nafasi ya Mrundi Ettienne Ndayiragijje aliyechukuliwa na klabu ya Azam FC ya nyumbani pia, kabla ya kuhamia timu ya taifa ya Tanzania.
  Na baada ya kutolewa hatua ya makundi kwenye Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame Julai mwaka huu nchini Rwanda, Mayanja akashindwa kuisaida KMC kufika mbali Kombe la Shirikisho Afrika kufuatia kutolewa na AS Kigali ya Raundi ya kwanza tu.
  Kutoka hapo,Mayanja ambaye awali alifundisha timu za Simba SC, Kagera Sugar ya Bukoba na Coastal Union ya Tanga kwa hapa Tanzania akaingia katika mwanzo mgumu kwenye Ligi Kuu ambao unahitimisha safari yake KMC.
  Mayanja ni kocha aliyeanzia kuwa mchezaji hodari kwao Uganda, ambako baada ya kuwa kiungo tegemeo wa timu ya taifa, The Cranes miaka ya 1980 hadi 1990 mwanzoni na klabu za KCCA ya Kampala akaenda kucheza soka ya kulipwa Misri, klabu ya El- Masry.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KMC YAMTUPIA VIRAGO MAYANJA MIEZI MITANO TU TANGU ARITHISHWE MIKOBA YA NDAYIRAGIJE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top