• HABARI MPYA

  Jumatatu, Novemba 04, 2019

  KAPOMBE ATANGAZA KUJIENGUA TAIFA STARS KWA SABABU YA MAUMIVU YA MARA KWA MARA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BEKI wa Simba SC, Shomari Kapombe ametangaza kustaafu kuichezea timu yake ya taifa ya Tanzania, ‘TaifaStars’ kwa sababu za kiafya.
  Katika taarifa yake ya jana, Kapombe amesema kwamba kutokana na kutetereka kwa afya yake kufuatia majeraha ya mara kwa mara ameona ni bora kustaafu kuchezea Taifa Stars na kutoa nafasi kwa wachezaji wengine.
  “Kutokana na kutetereka kwa afya yangu kufuatia majeraha ya mara kwa mara, nimeona sasa ni wakati muafaka wa kustaafu kuchezea Taifa Stars na kutoa nafasi kwa wachezaji wengine kuitumikia timu yetu,”.
  Kapombe amesema yuko tayari kurejea kwenye timu hiyo wakati wowote afya yake itakapoimarika.

  “Pamoja na hayo nipo tayari kurejea kuitumikia Taifa Stars kama kijana mzalendo wa taifa hili tukufu pale nitakapoona afya yangu imeimarika na kwamba mchango wangu katika kikosi hicho utakuwa wenye mafanikio chanya,” imeeleza sehemu ya taarifa iliyotolewa leo na mchezaji huyo kwa umma.
  Kapombe aliumia Novemba 16, mwaka jana mjini Bloemfontein, Afrika Kusini ambako Taifa Stars ilikuwa imeweka kambi kujiandaa na mchezo dhidi ya Lesotho, Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zilizofanyika Juni mwaka huu nchini Misri.
  Na tangu hapo Kapombe hakuwahi kuchezea tena Taifa Stars japo ameendelea kuitwa na wakati wote amekuwa akijitoa, au kuenguliwa kwa sabababu ya maheruhi.
  Mei 1, mwaka huu alijumuishwa kwenye kikosi cha awali cha wachezaji 39 kwa ajili ya Fainali za AFCON na kocha wa Taifa Stars wakati huo, Emmanuel Amunike, lakini hakuwahi kuripoti kambini kwa sababu zaa maumivu.
  Kocha mpya, Mrundi Etienne Ndayiragije akamrejesha kikosini Kapombe kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji, Rwanda uliofanyika mjini Kigali Oktoba 14, lakini kwa mara nyingine beki huyo hakujiunga na timu kwa sababu za kiafya pia.
  Na sasa anatoa tamko la kujiuzulu wakati Ndayiragije anatarajiwa kutaja kikosi kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Kundi J kufuzu AFCON ya 2021 nchini Cameroon dhidi ya Equatorial Guinea Novemba 15 mjini Dar es Salaam, ambao utafuatiwa na mchezo wa ugenini dhidi ya Libya Novemba 19.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KAPOMBE ATANGAZA KUJIENGUA TAIFA STARS KWA SABABU YA MAUMIVU YA MARA KWA MARA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top