• HABARI MPYA

  Ijumaa, Aprili 21, 2017

  VIONGOZI YANGA ‘WAISUSA’ TIMU, BENCHI LA UFUNDI MAJI YA SHINGO

  Na Steven Kinabo, DAR ES SALAAM
  HAKUNA kiongozi yeyote aliyefika mazoezini au hata kukutana na ama makocha au wachezaji wa Yanga tangu timu imerejea kutoka Algeria, ambako Jumamosi ilitolewa kabisa katika michuano ya Afrika.
  Yanga ilifungwa 4-0 na Mouludia Club Alger mjini Algiers Jumamosi katika mchezo wa marudiano wa mchujo wa kuwania kwenda hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na kutolewa kwa jumla ya mabao 4-1 kufuaatia kushinda 1-0 kwenye mchezo wa kwanza Dar es Salaam.
  Na tangu timu imerejea Jumanne na kuanza mazoezi ya kujiandaa na mechi zake za mashindano ya nyumbani ni kama viongozi wameisusa.
  Na kwa ujumla tangu Mwenyekiti Yussuf Manji awatembelee mazoezini siku moja ya kabla ya kwenda Algiers hawajaonana na kiongozi mwingine yeyote ukiondoa Katibu Mkuu, Charles Boniface Mkwasa waliyekuwa naye Algeria.  
  Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji (kushoto) na Makamu wake, Clement Sanga (kulia)

  Wachezaji wanalalamika viongozi wamewatelekeza na wanafanya mazoezi bila kupata hata posho achilia mbali madai yao ya mishahara ya miezi mitatu.
  Hali hiyo inafanya benchi la Ufundi linaelemewa na majukumu, kwani kabla ya kufikiria kufundisha timu inabidi waaanze kufikiria namna ya kuwabembeleza wachezaji, ambao kwa kiasi kikubwa wamekatishwa tamaa.
  Wachezaji wanakubali timu inakabiliwa na hali ngumu kwa sasa tangu kupata matatizo kwa Mwenyekiti wao, Yussuf Manji lakini wanasikitika hawaoni jitihada za uongozi katika kukabiliana na hali hiyo.
  Na zaidi wanasikitika viongozi wamewatelekeza kabisa na hawamuoni kiongozi yeyote japo kuwatia moyo katika kipindi hiki kigumu.
  Hali hiyo imefanya idadi ya wachezaji wanaogoma kuongezeka na hata wanaofanya mazoezi kutofanya kwa ari.
  Na haya yanatokea wakati klabu inakabiliwa na mtihani wa kutetea mataji yake ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC).
  Jumamosi Yanga watakuwa wenyeji wa Prisons ya Mbeya katika mchezo wa kiporo wa Robo Fainali ya Kombe la ASFC Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, kuwania kuungana na Azam FC, Mbao FC na Simba SC ambazo tayari zimetinga Nusu Fainali.
  Lakini kuelekea mchezo huo, benchi la Ufundi linaonekana kukata tamaa kutokana na viongozi kuisusa timu huku wachezaji wakionekana kabisa kufikia tamati ya uvumilivu wao.
  Katibu Mkuu wa Yanga hakupatikana mapema kuzungumzia hali hiyo, lakini Bin Zubeiry Sports – Online itaendelea kumtafuta ili kujua kutoka upande wake. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: VIONGOZI YANGA ‘WAISUSA’ TIMU, BENCHI LA UFUNDI MAJI YA SHINGO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top