• HABARI MPYA

    Tuesday, April 18, 2017

    JEONESIYA RUKYAA ATOA USHAHIDI

    Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
    REFA maarufu wa kike wa kimataifa nchini, Jonesiya Rukyaa ametoa ushahidi wake mbele ya Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juu ya sakata la beki Mohammed Fakhi kuichezea Kagera Sugar dhidi ya timu yake ya zamani, Simba akiwa ana kadi tatu za njano.
    Rukyaa aliyekuwa refa wa akiba katika mchezo ambao inadaiwa Fakhi alipata kadi nyingine ya njano kukamilisha tatu dhidi ya African Lyon Jumatano ya Januari 18, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba amefuta utata.
    “Rukyaa ametoa ushahidi wake ambao umefanana na wa Kamisaa, kwamba Fakhi hakupewa kadi ya njano Januari 18. Na muda ambao refa anasema alimuonyesha kadi ya njanoi Fakhi tayari alikuwa amekwishatoka uwanjani baada ya kuumia,”kimesema chanzo kutoka kwenye kikao cha Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF kinachoendelea hivi sasa hoteli ya Protea, Masaki, Dar es Salaam.
    Jonesiya Rukyaa amesema Mohammed Fakhi hakuwa na kadi tatu za njano

    Kikao hicho kinafuatia Kagera Sugar kupinga uamuzi wa Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72 kuipa Simba SC pointi tatu na mabao matatu kutokana na Rufaa waliyoikatia timu hiyo kwa madai ya kumtumia Fakhi akiwa ana kadi tatu za njano katika mechi baina ya timu hizo Aprili 2, mwaka huu.
    Katika barua iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Kagera Sugar, Hamisi Madaki kuelekea kwa Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa, klabu hiyo imeliomba shirikisho hilo kupitia upya maamuzi ya Kamati ya Saa 72 kwa kuwa Fakhi hakuwa na kadi tatu za njano kama ilivyodaiwa.
    Ikumbukwe Simba iliwasilisha malalamiko ikitaka ipewe ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kutokana na Kagera Sugar kumchezesha Fakhi akiwa na kadi tatu za njano katika mechi yao namba 194 iliyofanyika Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JEONESIYA RUKYAA ATOA USHAHIDI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top