• HABARI MPYA

  Jumamosi, Aprili 29, 2017

  SERIKALI YATANGAZA NIA YA KUZALISHA MABILIONEA WANAMICHEZO

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kwamba Serikali sasa imeanza mchakato wa kutengeneza mabilionea kupitia sekta ya Michezo ili baadaye waje kuisaidia nchi yao kutokana na utajiri wao.
  Waziri Mkuu ameyasema hayo usiku wa Ijumaa katika hoteli ya Serena, Dar es Salaam wakati wa hafla maalum ya kuichangia timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali, akiwemo Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.
  “Tumejifunza vya kutosha jinsi michezo inavyotoa mabilionea kwenye nchi mbalimbali duniani, ambao wanachangia pia maendeleo ya nchi yao kwa kiasi kikubwa kwenye uchumi wa nchi hizo, hivyo nasi hatuna budi kupita njia hiyo hiyo na sasa naamini kwamba tumeanza, na sasa tuendelee hivyo,”amesema Waziri Mkuu.
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa hafla ya kuichangia Serengeti Boys usiku wa Ijumaa mjini Dar ea Salaam

  Zaidi ya Sh. Milioni 200 zimechangwa usiku huo katika hafla hiyo kwa ajili ya Serengeti Boys inayotarajiwa kushiriki Fainali za U-17 Afrika nchini Gabon Mei mwaka huu.
  Na Waziri Mkuu akawahamasisha Watanzania kuchangia zaidi ili kutimiza lengo la upatikanaji wa Sh. Bilioni 1 zisaidie ushiriki wa timu hiyo kwenye fainali hizo zinazotarajiwa kuanza Mei 14 hadi 28, mwaka huu nchini Gabon.
  Kwa upande wake, Waziri Mwakyembe kama Mwenyekiti wa Kamati ya kuhamasisha watu kuchangia timu hiyo, Charles Hillary aliwapongeza waliojitokeza kuichangia Serengeti Boys na akaomba wengine wachangie ili kutimiza lengo la upatikanaji wa Sh. Bilioni 1.
  Waziri Mkuu, Majaliwa alihitimisha shughuli hiyo kwa kwenda kupiga penalti kumfunga mchezaji wa kipekee kuwahi kutokea kwenye soka ya Tanzania, Kitwana Manara aliyeanza kama kipa hodari miaka ya 1960 na baadaye kugeuka kuwa mshambuliaji hatari miaka 1970.
  Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi alisema timu imeandaliwa vizuri kwa ajili ya fainali hizo na ni matarajio yake itatimiza dhamira ya kupata tiketi ya kwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini India.
  Tayari Serengeti Boys ipo mjini Younde, Cameroon tangu jana baada ya kambi takriban mwezi mmoja mjini Rabat, Morocco ambako pia ilipata mechi mbili za kirafiki za kujipima nguvu dhidi ya Gabon na kushinda 2-1 kila mchezo.
  Kwa ujumla Serengeti Boys imekwishacheza mechi tano tangu kuanza kambi rasmi ya maandalizi fainali za Gabon, baada ya awali kuifunga Burundi mara mbili, Machi 30 mabao 3-0 na Aprili 1 mabao 2-0, mechi zote mbili zikipigwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, kabla ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Ghana ‘Black Starlets’ Aprili 3 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Ikisa mjini Younde, Serengeti Boys inatarajiwa kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya wenyeji, Cameroon Mei 3 na 6, mwaka huu kabla ya Mei 7 kwenda Gabon ambako imepangwa kundi B pamoja na timu za Mali, Niger na Angola.
  Cameroon nayo itashiriki fainali hizo ikiwa imepangwa Kundi A lina timu za wenyeji, Gabon, Guinea na Ghana. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SERIKALI YATANGAZA NIA YA KUZALISHA MABILIONEA WANAMICHEZO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top