• HABARI MPYA

  Jumapili, Aprili 30, 2017

  SERENGETI BOYS YAWAPIGA CAMEROON 1-0 KWAO

  Na Mwandishi Wetu, YAOUNDE
  TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys imeendeleza wimbi la ushindi katika mechi zake za kujipima nguvu baada ya leo kuwafunga wenyeji, Cameroon 1-0 mjini Yaounde.
  Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Ahmadou Ahijo, mjini Yaounde na kuhudhuriwa na gwiji wa soka wa Cameroon, Rogger Milla, bao la Serengeti Boys limefungwa na Ally Ng'anzi dakika ya 36.
  Serengeti Boys ilitua Younde, Cameroon Alhamisi ikitokea mjini Rabat, Morocco ambako iliweka kambi ya karibu mwezi mmoja na kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Gabon na kushinda 2-1 kila mchezo.
  Kwa ujumla Serengeti Boys imekwishacheza mechi tano tangu kuanza kambi rasmi ya maandalizi fainali za Gabon, baada ya awali kuifunga Burundi mara mbili, Machi 30 mabao 3-0 na Aprili 1 mabao 2-0, mechi zote mbili zikipigwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, kabla ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Ghana ‘Black Starlets’ Aprili 3 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Baada ya mchezo wa leo, Serengeti Boys inatarajiwa kurudiana na Cameroon Mei 3, mwaka huu kabla ya Mei 7 kwenda Gabon ambako imepangwa kundi B pamoja na timu za Mali, Niger na Angola.
  Cameroon nayo itashiriki fainali hizo ikiwa imepangwa Kundi A lina timu za wenyeji, Gabon, Guinea na Ghana. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SERENGETI BOYS YAWAPIGA CAMEROON 1-0 KWAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top