• HABARI MPYA

  Jumamosi, Aprili 29, 2017

  AZAM FC WALIA NA REFA, WADAI AKRAMA KAWABEBA SIMBA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KOCHA Msaidizi wa Azam FC, Iddi Nassor Cheche ameponda uchezeshaji wa refa Mathew Akrama katika Nusu Fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), michuano inayojulikana kama Azam Sports Federation Cup (ASFC).
  Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo, Simba SC imeshinda 1-0 bao pekee la kiungo Mohammed ‘Mo’ Ibrahim dakika ya 48 – na Cheche akasema wapinzani wao ‘walibebwa’ na refa Akrama.
  Refa Mathew Akrama akisindikizwa na wana usalama baada ya mechi leo 

  Cheche alianza kwa kukandia kadi nyekundu ya mapema ambayo Akrama alimuonyesha kiungo wa Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ akisema haikuwa halali na akasema maamuzi mengi ya refa huyo leo yalikuwa ya utata.
  Alisema dalili za kutotendewa haki katika mchezo huo walianza kuziona tangu mapema asubuhi katika kikao cha kabla ya mechi na akawatahadharisha wachezaji wake kuwa makini.
  Pamoja na hayo, Cheche amekubali matokeo, Azam FC ikipoteza nafasi ya mwisho ya kukata tiketi ya kucheza michuano ya Afrika kupitia Kombe la ASFC na akasema wanakwenda kujipanga kwa ajili ya msimu ujao.
  Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa Simba, Mganda Jackson Mayanja alikataa kuzungumzia maamuzi ya refa akisema kwamba hiyo si taaluma yake na hajasomea.
  Mayanja akasema baada ya ushindi huo wanaelekeza nguvu zao kwenye mchezo wa fainali, ambako watakutana na mshindi kati ya Mbao FC na Yanga zinazomenyana kesho katika Nusu Fainali ya pili.
  Mbali na Sure Boy kutolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja dakika ya 15, baada ya kugongana na mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Hajib, mshindi wa mechi ya leo, Mo Ibrahim naye alionyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 77 baada ya kumchezea rafu beki wa Azam FC, Shomary Kapombe.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC WALIA NA REFA, WADAI AKRAMA KAWABEBA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top