• HABARI MPYA

  Jumapili, Aprili 23, 2017

  IPO HAJA YA JUMA KASEJA KUREJESHWA TAIFA STARS

  AISHI Manula alisimama langoni wakati Tanzania inaifunga Botswana 2-0 Machi 25 katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Na Machi 28 Deogratius Munishi ‘Dida’ akasimama langoni wakati Taifa Stars inaifunga Burundi 2-1 katika mchezo mwingine wa kirafiki Uwanja huo huo, wa Taifa, kocha Salum Mayanga akianza vizuri kuvaa viatu vya Charles Boniface Mkwasa.
  Taifa Stars ilishinda mechi zote, lakini bila shaka ni kutokana na ubutu wa safu za washambuliaji za wapinzani, wetu kwani makosa ya safu zote za ulinzi na makipa kwa ujumla katika mechi zote mbele ya washambuliaji makini ni hatari.
  Makipa wote, Aishi na Dida wameshuka viwango kwa sasa kutoka kwenye ubora waliokuwa nao miaka miwili iliyopita.
  Safu ya ulinzi ya Stars nayo imeyumba kwa sasa – beki wa kulia chaguo la kwanza kwa muda mrefu, Shomary Kapombe anajaribu kurejea uwanjani taratibu baada ya kuwa nje kwa muda mrefu sababu ya matatizo ya kiafya na aliyekuwa chaguo la tatu, Hassan Kessy sasa ndiye anayeelekea kuchukua nafasi.
  Beki chaguo la pili Juma Abdul naye anajaribu kurejea uwanjani baada ya kuwa nje pia kwa sababu za majeruhi kwa muda mrefu. Beki wa kushoto, Mwinyi Hajji Mngwali anameguka kutokana na Zanzibar kupata uanachama wa kudumu wa Shrikisho la Soka Afrika (CAF) na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ amechukua nafasi.
  Mabeki wote wa kati, Kevin Yondan na aliyekuwa Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wamejitoa kwenye timu. Lakini pia Cannavaro angeondoka kwa lazima baada ya Zanziabr kupata uanachama wa CAF.
  Mechi na Botswana Mayanga aliwapanga mkongwe Erasto Nyoni na chipukizi Abdi Banda kucheza pamoja beki ya kati. Mechi na Burundi, Erasto ambaye nguvu na kasi yake vimepungua kutokana na umri pia aliwekwa nje na badala yake akacheza Salim Mbonde.
  Bila shaka Mbonde na Banda ndiyo ukuta mpya wa Taifa Stars kuanzia sasa na mwalimu anapaswa kuwafanyia kazi ili waweze kucheza pamoja na pia wapunguze makosa. Lakini anapaswa kuwa na wabadala wao vijana wadogo zaidi yao katika benchi.       
  Wachezaji wa nafasi za kiungo kwa sasa wapo wengi, bahati mbaya anakosekena kiungo hodari wa ulinzi na katika hilo tutalazimika kusubiri akina Himid Mao na Jonas Mkude wapate uzoefu zaidi.
  Viungo wachezeshaji wapo akina Said Ndemla na Muzamil Yassin, ingawa wanahitaji kuongeza vitu fulani muhimu na kupunguza vitu visivyo vya lazima, ili wajiongezee sifa za viungo bora wa kisasa wachezeaha timu.
  Vipi kuhusu langoni? Aishi na Dida wameshuka viwango na ukiwafananisha na kipa wa tatu aliyeitwa na Mayanga kwenye kikosi kilichopita, bado wanabaki kuwa bora.
  Na ukirejea kwenye klabu zao unagundua wote Aishi kwa Azam na Dida Yanga hawana washindani wa kuwafanya waongeze juhudi, hivyo ni kama wamebweteka.
  Kipa pekee ambaye anaweza kuwapa changamoto Aishi Manula na Dida ni mkongwe Juma Kaseja wa Kagera Sugar.
  Kaseja bado kipa bora na anastahili siyo tu kurudi timu kubwa, bali pia kurejeshwa timu ya taifa na akawa kipa chaguo la kwanza bila wasiwasi wowote hadi hapo Aishi na Dida watakapokuwa tayari tena kumuondoa.  
  Haitakuwa ajabu Kaseja kurudishwa timu ya taifa kama uwezo wake uliomfanya hadi achaguliwe mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa mwezi Januari, mwaka huu utamridhisha kocha Mayanga pia. 
  Kaseja amekuwa akidaka kwa kiwango kizuri Kagera Sugar tangu asajiliwe dirisha dogo Desemba mwaka jana na kuisaidia timu hiyo kupanda hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Na hiyo ni kwa sababu makipa wamekuwa na maisha marefu ya uwanjani tofauti na wachezaji wa nafasi nyingine.
  Mfano ni kipa wa kimataifa wa Misri, Essam El-Hadary ambaye Februari mwaka huu alikaribia kuipa nchi yake Kombe la Mataifa ya Afrika akiwa ana umri wa miaka 44. 
  Ikumbukwe Januari mwaka 2013 El-Hadary alitangaza kustaafu soka ya kimataifa baada ya kuwekwa, benchi mfululizo.
  Mchezaji huyo wa 23 kucheza mechi nyingi za timu yake ya taifa kihistoria ambaye pia ndiye mshindi wa mataji mengi ya Kombe la Mataifa ya Afrika, alirejea kikosi cha Mafarao katika mchezo dhidi ya Bosnia Herzegovina Machi 5, 2014 wakishinda 2–0.
  Juni 4 mwaka 2016, El-Hadary alidaka kwa dakika zote 90 Misri ikitufunga 2-0 Tanzania kwenye mchezo wa kufuzu AFCON Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
  Na Januari 17 mwaka huu, siku mbili baada ya kufikisha umri wa miaka 44, akaweka rekodi ya kuwa mchezaji mkubwa zaidi daima kucheza mechi ya AFCON baada ya kuchukua nafasi ya Ahmed El-Shenawy kwenye mechi ya kwanza ya Misri katika mashindano.
  Februari 1, mwaka huu El-Hadary akaokoa mikwaju miwili ya penalti Misri ikiifunga Burkina Faso kwa penalti 4-3 kwenda fainali ya AFCON 2017 ambako walifungwa na Cameroon walioibua mabingwa kwa ushindi 2-1.
  Kwa ujumla, hadi sasa El-Hadary ameichezea Misri mechi 144, akishinda mataji manne ya AFCON na alikuwa kipa bora wa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2006 katika fainali za nyumbani, Misri.
  Kwa ubora wa Kaseja kwa sasa na kushuka kwa viwango vya akina Aishi na Dida, ipo haja ya Kaseja kurejeshwa Taifa Stars. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: IPO HAJA YA JUMA KASEJA KUREJESHWA TAIFA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top