• HABARI MPYA

  Alhamisi, Aprili 20, 2017

  MARAIS WA VYAMA SOKA UKANDA WA CECAFA WAAZIMIA MAKUBWA

  MARAIS wa vyama na mashirikisho ya soka ya nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) wamekutana mjini Kampala, Uganda kujadili maendeleo ya soka ya ukanda wao.
  Mkutano huo uliopata mahudhurio mazuri ambao ulifanyika mabao makuu ya Shirikisho la Soka Uganda (FUFA), Mengo, ulilenga kujadili namna ya kuinua soka ya ukanda huu.
  Marais saba wa ukanda huo, akiwemo mwenyeji Mhandisi Moses Magogo walikuwemo kwenye chumba cha mikutano jengo la FUFA.
  Kutoka kushoto Ravia Faina wa Zanzibar, Nicholas Mwendwa wa Kenya, Ndikuniyo Reverien wa Burundi, Mhandisi Moses Magogo wa Uganda, Juneidi Tilmo wa Ethiopia, Vincent Nzamwita wa Rwanda na Jamal Malinzi wa Tanzania katika kikao chao ofisi za FUFA jana

  Marais wa ukanda wa CECAFA waliohudhuria kikao hicho ni Vincent Nzamwita wa Rwanda, Jamal Malinzi wa Tanzania, Juneidi Tilmo wa Ethiopia, Nicolas Mwendwa wa Kenya, Ndikuniyo Reverien wa Burundi na Ravia Faina wa Zanzibar.
  Marais wa Sudan Kusini, Sudan na Djibouti walikosekana baada ya kutoa taarifa mapema za udhuru.
  Mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na marekebisho ya Katiba ya CECAFA, kushinikiza Mkutano Mkuu wa CECAFA haraka iwezekanavyo, kuhakikisha CECAFA inakuwa na makao makuu ya kudumu, kuboresha mashindano ya CECAFA kuanzia ya vijana chini ya umri wa miaka 15, U-17 na U-20 kwa wavulana na wasichana na soka la ufukweni.
  Mengineyo ni kuboresha mambo ya kiufundi katika mchezo kama Urefa, Ukocha, Utawala na Tiba, kuboresha Masoko, Mawasiliano na kutengeneza upya nembo ya kibiashara ya CECAFA.
  Imekubaliwa pia ukanda huu kuwasilisha ombi rasmi la kuwa mwenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika hivi karibuni, kuhakikisha CECAFA inakuwa na wajumbe wa maana kwenye Kamati ya Utendaji ya CAF, kutengeneza wazo la kuomba fedha FIFA kusaidia maendeleo ya soka kwa ukanda huu kuanzia kwenye soka ya vijana, wanawake na ufukweni.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MARAIS WA VYAMA SOKA UKANDA WA CECAFA WAAZIMIA MAKUBWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top