• HABARI MPYA

  Jumapili, Aprili 30, 2017

  VIONGOZI AZAM FC WAJITATHMINI BAADA YA MATOKEO MABAYA ZAIDI NDANI YA MIAKA MITANO

  KIPIGO cha bao 1-0 kutoka kwa Simba jana katika Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Azam Sports Federation Cup (ASFC) kinaifuta Azam FC katika michuano ya Afrika mwakani.
  Kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitano Azam FC itakosekana kwenye michuano ya Afrika, ikitoka kushiriki Ligi ya Mabingwa mara moja na Kombe la Shirikisho mara nne.
  Unaizungumzia timu yenye bajeti kubwa zaidi ya uendeshwaji kutokana na kuajiri wachezaji na makocha wa gharama kubwa, wanaolipwa vizuri.
  Timu yenye viongozi wote wanaolipwa mishahara kwa sababu ni waajiriwa wa kampuni ya Said Salim Bakhresa, wamiliki wa Azam FC na si wa kuchaguliwa na wanachama wanaofanya kazi kwa ridhaa na utashi.
  Timu pekee yenye Uwanja wake rasmi ulioidhinishwa hadi na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa mechi za kimataifa.
  Azam FC ndiyo klabu mfano wa kuigwa nchini na hiyo ndiyo klabu kubwa zaidi kwa thamani na hadhi nchini, ukiachilia mbali ukubwa wa majina na umaarufu wa Simba na Yanga.
  Azam hakikosekani kitu. Wachezaji siyo tu wanalipwa vizuri, bali wanalipwa kwa wakati – yaani wamiliki wanaihudumia timu vizuri, hakuna shaka.
  Upande wa pili, wachezaji wa Simba na Yanga wanatamani huduma ambazo wanazipata wachezaji wa Azam FC. Mara kadhaa wachezaji Yanga wamegoma msimu huu kushinikiza walipwe malimbikizo ya mishahara yao ya miezi kadhaa.
  Lakini pamoja na yote Yanga wanawania ubingwa wa Ligi Kuu na jioni ya leo wanaweza kujihakikishia tiketi ya michuano ya Afrika mwakani tena kama wataifunga Mbao FC katika Nusu Fainali ya pili ya Kombe la ASFC.
  Azam wamekwishatupwa nje ya mbio za ubingwa wa Ligi Kuu na jana wametolewa kwenye Kombe la ASFC katika msimu ambao wamiliki walitoa fedha nyingi mno kusajili wachezaji wapya na makocha wapya.
  Mwanzoni mwa msimu Azam ilileta jopo la makocha kutoka Hispania chini ya Zeben Hernandez Rodriguez, ambao walifukuzwa baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu na kuletwa Mromania Aristica Cioaba.
  Waspaniola walianza vizuri kwa kuipa timu ya Ngao ya Jamii, lakini wakawa na mwendo wa kusuasua kidogo kwenye Ligi Kuu hata ikawa sababu ya kufukuzwa kwao, lakini bahati mbaya mbadala wao naye hajafanya vizuri.
  Msimu huu Azam imebadili wachezaji wote wa kigeni, wakiondoka Waivory Coast Kipre Balou, Kipre Tchetche, Serge Wawa, Mrundi Didier Kavumbangu, Mkenya Alan Wanga na Mnyarwanda Jean Baptiste Muguraneza.
  Mwanzoni mwa msimu walisajiliwa Ya Thomas Renaldo kutoka Ivory Coast, 
  Daniel Amoah kutoka Ghana, Francesco Zekumbawira, Bruce Kangwa wote kutoka ambao waliungana na Mugiraneza, Wawa na Balou kukamilisha idadi ya wachezaji saba wa kigeni.
  Lakini katika dirisha dogo Desemba wakaachwa wote na kubaki Daniel Amoah na Bruce Kangwa waliounganishwa na Samuel Afful, Daniel Atta Agyei, Yahaya Mohammed, Yakubu Mohammed wote kutoka Ghana na Stephan Kingue kutoka Cameroon.
  Zote hizo ni fedha ambazo Said Salim Bakhresa ilizitumia katika mradi ambao bado haujaanza kujiendesha. 
  Kampuni pia iliongeza nguvu upande wa Watendaji baada ya kuajiriwa Meneja Mkuu, Abdul Mohammed na watendaji wengine wadogo wadogo.
  Lakini mwisho mwa msimu, timu inakosa nafasi ya kucheza michuano ya Afrika mwakani kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitano.
  Si haba, imetwaa mataji mawili, kwani mbali na kuifunga Yanga katika Ngao ya Jamii, pia iliifunga Simba katika fainali ya Kombe la Mapinduzi, lakini mataji hayo yanawapeleka wapi?
  Bila shaka, Azam FC ipo katika msimu mbaya zaidi ndani ya miaka mitano na hii inamaanisha kuna haja ya viongozi wa Azam FC kujitathmini, walikosea wapi?
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: VIONGOZI AZAM FC WAJITATHMINI BAADA YA MATOKEO MABAYA ZAIDI NDANI YA MIAKA MITANO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top